Rais wa Marekani, Donald Trump, amedai kwamba nchi hiyo itashinda kama itaingia vitani na nchi yoyote.
Donald Trump alidai Jumanne wiki hii kwamba nchi hiyo itashinda iwapo itaingia vitani na nchi yoyote, bila kutaja vita visivyoisha vya Washington katika miaka ya hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na kukimbia na kuondoka kwa aibu na madhila huko Afghanistan na Iraq. Tump amesema katika hotuba yake ndani ya meli ya kubeba ndege za kivita ya USS George Washington karibu na Tokyo, kwamba: “Kuanzia sasa, tukienda vitani, tutashinda.”
Trump amesisitiza umuhimu wa kutumia nguvu kwa ajili ya kueneza amani duniani na kuongeza kuwa: “Tofauti na tawala zilizopita, hatutatenda kisiasa.”
Rais wa Marekani amesema yuko tayari kutumia jeshi na Gadi ya Taifa kudumisha usalama wa miji ya Marekani na atatumia vikosi vyote vya jeshi iwapo itahitajika.
Madai yasiyo na msingi ya Trump kuhusu kushinda Marekani katika vita vyote yanapingana na ukweli uliothibitishwa wa vita viwili vikubwa ambavyo Marekani ilianzisha nchini Afghanistan mwaka wa 2001 na Iraq mwaka wa 2003. Agosti 2021, katika mwaka wa kwanza wa urais wa Joe Biden, Marekani iliondoa haraka vikosi vyake vya jeshi huko Afghanistan baada ya miaka 20 ya kuikalia kwa mabavu nchi hiyo, na ukweli ni kwamba, wanajeshi wa Marekani walikimbia Afghanistan. Marekani ilipoteza karibu wanajeshi 2,500 katika vita vyake virefu zaidi, yaani vita vya Afghanistan. Kuondolewa vikosi vya jeshi la Marekani huko Afghanistan kwa amri ya Biden, ambako hatimaye kulipelekea kuanguka serikali ya nchi hiyo, na kundi la Taliban likashika hatamu za uongozi wa Afghanistan, kuliibua ukosoaji mkubwa kutoka ndani na nje ya nchi. Licha ya ukosoaji huo, Joe Biden alisisitiza kwamba amechua uamuzi sahihi wa kuwaondoa wanajeshi wa Marekani huko Afghanistan. Katika hotuba yake ya kwanza baada ya kuondolewa wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan, Biden alikiri kwamba vita hivyo vilikuwa vikiigharimu Marekani dola milioni 300 kwa siku kwa miongo miwili na kwamba Washington ilikuwa ikikabiliwa na machaguo mawili: Ama kuondoa Afghanistan au kuongezeka kwa mzozo wa kijeshi.

Haraka ya Biden katika kuwaondoa wanajeshi wa Marekani huko Afghanistan ilikuwa sawa kabisa na kile kilichotokea wakati wanajeshi wa Marekani walipoondoka Vietnam. La kupewa mazingatio hapa ni kwamba, mnamo Aprili 2025, Donald Trump alikosoa jinsi wanajeshi wa Marekani walivyoondoka Afghanistan, na kulitaja tukio hilo kuwa ni “fedheha kubwa zaidi katika historia ya Marekani”. Alidai kwamba kama angekuwa rais, janga hilo lisingetokea kamwe.
Kuhusu Iraq, mashambulizi na uvamizi wa Marekani nchini humo mwaka 2003 ulikuwa na matokeo mabaya sana kwa serikali ya Washington. Uvamizi wa kijeshi nchini Iraq, mbali na kusababisha maafa makubwa kwa watu wa Iraq, ulisababisha vifo vya maelfu ya wanajeshi wa Marekani, gharama kubwa kwa uchumi wa nchi hiyo na sifa mbaya kimataifa. Kwa mujibu wa data za Pentagon, jumla ya wanajeshi 4,487 wa Marekani waliuawa katika vita vya Iraq. Wakati wa muhula wake wa kwanza kama rais, Donald Trump alisema katika hotuba yake mnamo Machi 2019 kwamba: “Tumetumia dola trilioni 7 Mashariki ya Kati, lakini hatuwezi kutua (kwa ndege) tukiwa tumewasha taa.” Trump alikuwa akiashiria safari yake ya siri nchini Iraq, ambapo alilazimika kufanya safari ya kushtukiza na isiyotangazwa, na ndege yake ikatua katika kambi ya kijeshi ya Marekani katika jimbo la Anbar ikiwa imezima taa.
Wakati wa urais wa Barack Obama hadi Desemba 2011, Marekani iliondoa zaidi ya wanajeshi 150,000 kutoka Iraq ili kuzuia mauaji na hasara zaidi. Hivi sasa, wanajeshi wapatao 2,500 wa Marekani bado wapo nchini humo katika kambi kadhaa.

Kwa ujumla, vita vya Afghanistan na Iraq vimeorodheshwa katika historia kama kushindwa kukubwa zaidi mara mbili katika historia ya kijeshi ya Marekani katika karne ya 21. Licha ya ukweli huu usiopingika, Trump sasa anadai kwamba Marekani imepata ushindi katika vita vyote. Kama Trump anaashiria vita vya awali vya Marekani, uzoefu wa Afghanistan na Iraq ni mifano miwili ya kushindwa kabisa kwa nchi hiyo. Na iwapo anamaanisha ushindi wa Marekani katika vita vya siku zijazo, hasa na nguvu kubwa za kijeshi kama vile China na Russia, hitimisho hili pia ni la mapema na ni dai lisilothibitishwa, ambalo halikuzingatia uwezo wa kijeshi wa wapinzani wa Washington.
