
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania INEC ilianza kutangaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 jana Alkhamisi, huku Tume ya Uchahguzi Zanzibar ZEC ikimtangaza Rais Hussein Ali Hassan Mwinyi kuwa mshindi wa urais wa Zanzibar matokeo ambayo yamesusiwa na chama kikuu cha upinzani Zanzibar cha ACT Wazalendo.
Sambamba na INEC na ZEC kutangaza matokeo ya uchaguzi wa Tanzania nzima pamoja na Zanzibar, vurugu za hapa na pale pia zimeendelea kuripotiwa katika maeneo mbalimbali ya Tanzania hasa jijini Dar es Salaam suala ambalo limemfanya Mkuu wa Majeshi ya Tanzania kulaani vitendo vya vurugu vinavyoendelea nchini humo na kuwataka wananchi wa Tanzania wawe watulivu wakati jeshi na vikosi vingine vya ulinzi na usalama vikiendelea kukabiliana na vurugu hizo.
Jenerali Jacob John Mkunda ametoa mwito huo wa utulivu kwenye hotuba yake iliyorushwa na televisheni ya taifa na kusisitiza kwa kusema: “Ni lazima utawala wa sheria uzingatiwe” na ameonya kwamba wahusika wote wa machafuko hayo watachukuliwa hatua.
Mkuu wa Jeshi la Tanzania vilevile amesema: “Jeshi linashirikiana na vyombo vingine vya usalama kudhibiti hali ya usalama… jeshi na vyombo vingine vya usalama vinashirikiana kudhibiti hali hiyo.”
Matokeo ya awali yanaonesha kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anaongoza katika maeneo kadhaa.
Kabla ya hapo Tume HHuru ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania INEC ilikuwa imesema kuwa itamtangaza mshindi wa urais katika kipindi cha saa 72 ikiwemo siku ya upigaji kura ya Jumatano, Oktoba 29, 2025.
