Mazungumzo ya siku kadhaa kati ya wajumbe wa Taliban na Pakistan mjini Istanbul yamemalizika kwa upatanishi wa serikali ya Qatar na Uturuki.

Hata hivyo kwa mujibu wa msemaji wa serikali ya Taliban, pande hizo mbili zimekubaliana kufanya mikutano mingine katika siku zijazo ili kujadili masuala yaliyosalia.

Zabihullah Mujahid, msemaji wa serikali ya Taliban, alitangaza kuwa mazungumzo kati ya wajumbe wa Afghanistan na Pakistan huko Istanbul yamekamilika baada ya siku kadhaa za mazungumzo.

Kulingana na yeye, mazungumzo hayo yalifanyika kwa ombi na kwa upatanishi wa Qatar na Uturuki, na lengo lake lilikuwa kutafuta suluhisho la kidiplomasia kwa masuala kati ya nchi hizo mbili jirani.

Taarifa iliyotolewa na serikali ya Taliban imesema: ” Afghanistan inaamini katika diplomasia na maelewano tangu mwanzo na ilianza mchakato wa mazungumzo kwa uaminifu na umakini mkubwa, kupitia uteuzi wa timu ya kina na ya kitaalamu, na imefuatilia hadi hatua hii kwa ushirikiano kamili na subira.”

Zabihullah Mujahid, msemaji wa serikali ya Taliban,

Taarifa hiyo pia ilisisitiza kuwa Afghanistan inataka uhusiano mzuri na Pakistan, na kwamba uhusiano huu unapaswa kuzingatia kanuni za “kuheshimiana, kutoingilia mambo ya ndani ya kila mmoja, na kutotishia upande wowote.”

Hivi karibuni kulizuka mapigano makali ya mpakani kati ya majeshi ya Afghanistan na Pakistan huku vikosi vya nchi hizo mbili vikishambuliana kwa kutumia silaha nzito.

Mapigano hayo yalipamba moto siku moja baada ya serikali ya muda ya Afghanistan inayoongozwa na Taliban kulituhumu jeshi la Pakistan kuwa lilikiuka anga ya mji mkuu Kabul na kuripua soko moja kwenye eneo la Margha lililoko katika jimbo la Paktika linalopakana na Pakistan.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *