Mkutano ulimulika jinsi ya kusaka fedha za kuwasaidia walioathiriwa vibaya na machafuko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Bwana Huang amesema, “kwa mtazamo wangu, mkutano huu ulikuwa na mafanikio kwa angalau sababu mbili. Mosi, kutokana na kiwango cha ushiriki na utofauti wa nchi na mashirika yaliyowakilishwa: Marais watatu wa nchi, mawaziri wengi, na Marais wawili wa zamani ambao wamewahi kuwa wasuluhishi katika michakato ya amani.”

Kulikuwepo pia na wawakilishi wa ngazi ya juu na maafisa wengine wakuu kutoka Muungano wa Afrika, (AU), Muungano wa Ulaya, (EU) Umoja wa Mataifa, pamoja na mashirika ya kibinadamu ya ndani na ya kimataifa, miongoni mwa wengine.

Mjumbe huyo Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema “utofauti huu wa washiriki unaonesha wazi kwamba mgogoro ulioko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na katika Ukanda wa Maziwa Makuu si mgogoro uliosahaulika, na kwamba jumuiya ya kimataifa bado imejizatiti kikamilifu.”

Ahadi ya dola bilioni 1.5 imepatikana

Sababu ya pili ya mafanikio ya mkutano huu ni kwamba “uliwawezesha wawakilishi wa jumuiya ya kimataifa na mashirika ya kibinadamu ya ndani na ya kimataifa kujadili hatua za kuchukuliwa ili kupunguza mateso ya wale walioathirika na mgogoro mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo — hasa kutokana na ongezeko la ahadi zilizotolewa wakati wa mkutano, takriban dola bilioni 1.5 kwa ajili ya mpango wa misaada ya kibinadamu.”

Sasa tugeuze ahadi iwe vitendo

Bwana Huang amesema kazi iliyosalia sasa ni kuzigeuza ahadi hizi kuwa vitendo na kuhakikisha kwamba misaada inawafikia haraka wale wanaohitaji.

Na zaidi ya yote, “ni lazima tuendelee kushirikiana ili kumaliza kabisa migogoro inayoendelea kurudiarudia katika sehemu hii ya dunia.”

Akizungumza kwa njia ya video wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutoa msaada zaidi kwa nchi hiyo, ambako zaidi ya watu milioni 21 wanahitaji msaada ili kuendelea kuishi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *