Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO amelaani taarifa iliyoripotiwa kuhusu kuuliwa wagonjwa na raia kufuatia kushtadi machafuko katika mji wa El Fasher nchini Sudan. Tedros Adhanom Ghebreyesus ametaka kuhitimishwa uhasama.

Shirika la Afya  Duniani limelaani kuuawa wagonjwa na raia wa kawaida kufuatia kushtadi machafuko katika mji wa El Fasher, Sudan na ametoa wito wa kuhitimishwa uhasama ili kuwalinda raia na wafanyakazi wa mashirika ya misaada ya kibinadamu na kudhamini huduma za afya na ufikishaji wa haraka wa misaada ya kibinadamu kwa wananchi. 

Wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) siku ya Jumapili waliudhibiti mji wa El-Fasher kufuatia mapigano makali kati yao na jeshi la Sudan, jiji ambalo lilikuwa likizingirwa na wanamgambo hao tangu mwezi Mei mwaka jana.

Hii ni katika hali ambayo, ripoti za ndani na nje ya Sudan zinaonyesha kuwa  wanamgambo wa RSF wameuwa watu wengi, wametekeleza mauaji ya kikabila na na kuwatesa raia katika mji wa El Fasher.  

Wagonjwa zaidi ya 460 na jamaa zao wanaaminika kuuawa katika Hospitali ya Wazazi ya Saud huko El Fasher kufuatia mashambulizi ya karibuni na kutekwa wafanyakazi wa sekta ya afya.

Jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSf wamekuwa wakipigana katika vita vya wenyewe kwa wenye tangu Aprili 2023; mzozo ambao umeuwa maelfu ya watu wa Sudan na kusababisha wengine zaidi ya milioni 15 kuwa wakimbizi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *