Sheikh Mkuu wa Chuo Kikuu cha al-Azhar cha Misri ameitaka Italia ilitambue rasmi taifa la Palestina.

Sheikh Ahmed Al-Tayyib, amesema hayo katika mazungumzo yake na Rais wa Italia, Sergio Mattarella, katika mkutano uliofanyika Roma na kubainisha kwamba, ni muhimu kwa taifa hilo la Ulaya kulitambua rasmi Taifa la Palestina.

Sheikh Al-Tayyib alionesha kuthamini msimamo wa wananchi wa Italia na mshikamano wao na Wapalestina, pamoja na maandamano yao makubwa kupinga mashambulizi yanayoendelea ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Aidha alisema, “Tunathamini msimamo wa kimaadili ulioonyeshwa na wananchi wa Italia, na tunatarajia Italia itaungana na mataifa mengine ya dunia yaliyolitambua rasmi Taifa la Palestina, ikiwa ni hatua ya kuelekea kuanzishwa kwa taifa huru la Palestina mji mkuu wake ukiwa Baytul Muqaddas.

Kadhalika alisisitiza kwamba Al-Azhar itaendelea kusimama kwa dhati katika kuimarisha amani, ujumbe wa msingi wa Uislamu, pamoja na kupambana na upotoshaji kuhusu dini kupitia majadiliano na ushirikiano na taasisi za kimataifa za kidini na kitamaduni.

Akikumbusha kutiwa saini kwa Hati ya Udugu wa Kibinadamu mwaka 2019 katika Abu Dhabi akiwa na marehemu Papa Francis, Sheikh Al-Tayyib alisema mpango huo unaendelea kuimarisha mazungumzo ya baina ya dini na juhudi za kupambana na ubaguzi, misimamo mikali, na hotuba za chuki.

Rais Mattarella alisifu juhudi za Sheikh Al-Tayyib katika kueneza amani na uhusiano wake wa karibu na Papa Francis, akieleza kuwa Hati ya Udugu wa Kibinadamu ni “nguzo muhimu katika kustawisha amani ya kimataifa na mazungumzo ya kidini.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *