Umoja wa Mataifa Ijumaa ya wiki hii umetoa wito kwa vyombo vya usalama nchini Tanzania kuacha kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kando na kuwataka walinda usalama kujizuia kutumia nguvu zaidi, Umoja wa Mataifa umetaka uchunguzi dhidi ya maandamano yaliogeuka kuwa ya vurugu wakati wa uchaguzi kufanyika.
Katika hatua nyengine, chama kikuu cha upinzani Chadema kimeliambia shirika la habari la AFP siku ya Ijumaa kwamba karibia watu 700 wameuawa katika kipindi cha siku tatu za vurugu za uchaguzi.

Ofisi ya haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa imesema imepokea taarifa zinazoweza kuthibitishwa za kutokea kwa vifo katika jiji kuu la kibiashara Dar es Salaam, Shinyanga kaskazini Magharibi na Morogoro Mashariki ambapo walinda usalama walitumia risasi za moto na mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji.
“Tunaguswa na vifo na majeruhi ambavyo vimetokea wakati wa uchaguzi nchini Tanzania,” imesema taarifa ya Msemaji wa Ofisi ya haki za binadamu ya UN Seif Magango.

“Tunatoa wito kwa walinda usalama kuacha kutumia nguvu zaidi ikiwemo kutumia silaha nzito nzito dhidi ya waandamanaji na kufanya juhudi kuzuia kuongezeka kwa hali ya wasiwasi. Waandamanaji wanastahili kuandamana kwa amani.” ilisema taarifa ya UN.
Uchaguzi wa siku ya Jumatano uligubikwa na vurugu wakati waandamanaji waliingia jijini Dar es Salaam na Miji mingine wakikabiliana na polisi pamoja na kushambulia vituo vya kupiga kura hatua iliyopelekea kukatwa kwa itaneti na kutangazwa kwa makataa ya watu kutembea.
