Maafisa wa Umoja wa Mataifa wameonya kuhusiana na ‘ukatili wa kutisha’ unaofanyika nchini Sudan.
Umoja wa Mataifa umesema kwamba mauaji hayafanyiki Darfur pekee na kwamba kuna umwagaji mkubwa wa damu unaoendelea pia katika jimbo la Kordofan na hivyo kuhatarisha shughuli za utoaji misaada kwa raia wa Sudan.
Maafisa wa Umoja wa Mataifa wameonya kwamba hali inayoendelea nchini Sudan ni ya ukatili mkubwa na ni kitisho kikubwa kutokana na mashambulizi yanayoendelea ya vikosi vya wanamgambo wa RSF wanaoongozwa na Hamdana Dagalo.
Hivi karibuni mji wa El-Fasher uliopo katika jimbo la Darfur uliangukia mikononi mwa RSF. Mkuu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Tom Fletcher amesema kuwa, eneo hilo kwa sasa linakabiliwa na maafa makubwa na mateso ya kibinadamu yasiyoelezeka.
Kudhibitiwa kwa mji wa El Fasher kunakuja baada ya zaidi ya miezi 18 ya kuzingirwa na kuzua hofu ya kurejea kwa ukatili uliolenga makabila miaka 20 iliyopita.

Fletcher ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba, mauaji hayafanyiki Darfur pekee na kwamba kuna umwagaji mkubwa wa damu unaoendelea pia katika jimbo la Kordofan na hivyo kuhatarisha shughuli za utoaji misaada kwa raia wa Sudan.
Wakati huo huo, zaidi ya wagonjwa 460 na watu walioandamana nao wameripotiwa kupatikana wameuawa katika hospitali ya uzazi huku kukiwa na ripoti za kuendelea ukatili dhidi ya raia huko El Fasher, Sudan.
Hayo yanjiri katika hali ambayo, Shirika la Afya Duniani (WHO) limethibitisha kuweko mashambulizi 185 dhidi ya maeneo ya huduma za afya nchini Sudan. Wafanyakazi wa masuala ya afya 1,204 wameshauawa na wengine 416 kujeruhiwa tangu vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi vilipoanza nchini Sudan mwezi Aprili 2023.
