
Umoja wa Mataifa umeitangaza kwamba zaidi ya Wasyria 400,000 wamelazimikia kukimbia makazi yao kutokana na ukandamizaji wa kidini na ulipizaji kisasi tangu Jolani alipoingia madarakani nchini Syria.
Televisheni ya Al-Mayadeen imenukuu taarifa ya Umoja wa Mataifa ikisema kwamba zaidi ya Wasyria 400,000 wamehama makazi yao kutokana na mauaji ya umati na ukatili wanaofanyiwa na magenge yenye uhusiano na utawala mpya wa nchi yao.
Televisheni hiyo imeongeza kuwa, awamu ya mpito ya Syria imezusha mawimbi mapya ya wakimbizi makazi yaliyosababishwa na ulipizaji kisasi, ukandamizaji wa kidini, migogoro ya wenyewe kwa wenyewe na uvamizi wa Israel katika maeneo ya kusini mwa Syria. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 430,000 walihama makazi yao nchini Syria kati ya mwezi Disemba 2024 na Julai 2025, na hakuna kundi kati ya makundi mbalimbali ya kidini na kikabila nchini humo ambalo limesalimika epushwa na machafuko ambayo yameenea katika maeneo tofauti ya Syria.
Taarifa ya Umoja wa Mataifa pia imesema kwamba idadi kubwa zaidi ya watu waliokimbia makazi yao imetokea katika jimbo la kusini la Suweida, ambako mapigano ya umwagaji damu yametokea sana hata katika miezi michache iliyopita.
Kwa mujibu wa Mtandao wa Haki za Binadamu wa Syria, zaidi ya watu 1,300 wameuawa katika ukandamizaji uliofanywa na magenge yenye uhusiano na serikalli huko Suweida huku takriba watu 400 kati yao wakiwa raia wa kawaida na wengi wao wakiwa wa dini ya Druze. Baadhi ya taarifa zinasema kuwa, idadi ya waliouawa ni kubwa zaidi ya hiyo. Ghasia katika maeneo mengine pia zimewalazimisha makumi ya maelfu ya Wasyria kukimbia makwao. Kwa mujibu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu milioni 12 kati ya milioni 23 wa Syria wamekimbia makazi yao ndani au nje ya nchi hiyo ya Kiarabu katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni.
