
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, hatuwezi kusimamisha urutubishaji urani na kwamba kile ambacho maadui hawakukipata kupitia vita hakiwezi kupatikana kwa njia ya kisiasa.
Sayyid Abbas Araqchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema hayo katika mahojiano na televisheni ya Al Jazeera akijibu vitisho vya utawala wa Kizayuni na kusema: Tumejiandaa kwa tukio lolote na tunatarajia jambo lolote lile kutoka kwa utawala wa Kizayuni.
Ameongeza kuwa: Utawala wa Kizayuni wa Israel hauwezi kuishambulia Iran bila ya idhini na uungaji mkono kamili wa Marekani. Netanyahu ni mhalifu wa kivita na amethibitisha kwamba Israel ni adui halisi wa eneo hilo.
Kuhusu mazungumzo, Araqchi amesema: “Tuko tayari kwa mazungumzo ya kutatua hali ya wasiwasi unaodaiwa kuwepo kwenye mpango wetu wa nyuklia na tuna uhakika ni mpango wa amani kikamilifu.”
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran vilevile amesema: “Hatutajadiliana na yeyote kuhusu mpango wetu wa makombora na hakuna mtu mwenye akili timamu anayeweza kukubali kupokonywa silaha.”
Amesema: Hatuwezi kusimamisha urutubishaji wa urani na tunasema wazi kwamba kile ambacho hakikupatikana kupitia vita, hakiwezi kupatikana kwa njia ya kisiasa.
Kuhusu uwezekano wa mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani, Araqchi amesema: Hatuna nia ya kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Washington.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuhusu mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Syria kwamba: Tunaunga mkono uhuru wa nchi ya Syria na kupatikana uadilifu katika eneo hili na tunalaani uchokozi wa Israel dhidi ya Syria.