Hata hivyo, wazo kwamba maendeleo yanapaswa kuwa yanayomlenga mtu, jumuishi na yenye haki, si jipya. Ni maono ambayo dunia ilikubaliana nayo miaka 30 iliyopita katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa mjini Copenhagen — maono ambayo bado yanagusa mioyo hadi leo.

Wiki ijayo, viongozi kutoka kote ulimwenguni watakutana mjini Doha, Qatar, kwa mkutano wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa wenye lengo la kufufua maono hayo. Kuanzia tarehe 4 hadi 6 Novemba, Mkutano wa Pili wa Dunia kuhusu Maendeleo ya Kijamii utawaleta pamoja Marais, Mawaziri, wawakilishi wa asasi za kiraia, na wataalamu ili kutathmini maendeleo, kushughulikia mapungufu sugu, na kuweka mwelekeo mpya wa pamoja.
Katika kiini chake kuna swali rahisi lakini lenye nguvu: tunawezaje kuhakikisha kwamba hakuna mtu anayeachwa nyuma?

Doha, mji mkuu wa Qatar.

© Unsplash/Rhiannon Elliott

Doha, mji mkuu wa Qatar.

“Mkutano huu unakuja katika wakati nyeti,” amesema Li Junhua, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Masuala ya Uchumi na Kijamii.

Amesema: “Tofauti za kijamii zinaongezeka. Imani kwa taasisi inapungua. Jamii zinahangaika kutokana na migogoro, mishtuko ya tabianchi, na mabadiliko ya haraka ya kiteknolojia. Hata hivyo, tunaona ubunifu wa kipekee, ustahimilivu na mshikamano. Huu ndio wakati wetu wa kujenga upya imani kati ya serikali na wananchi wao — na kati ya mataifa.”

Wito wa kimataifa wa kuchukua hatua

Bjørg Sandkjær, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Masuala ya Uchumi na Kijamii, amesema kuwa mkutano huu ni “wito wa kimataifa wa kuchukua hatua” katika wakati ambapo zaidi ya watu bilioni moja bado wanaishi katika umaskini wa kupindukia na asilimia 40 ya watu duniani hawana ulinzi wa kijamii.

Ameiambia Idhaa ya Umoja wa Mataifa kwamba mkutano huu unalenga kufufua imani katika maendeleo ya pamoja — “imani kwamba tunaweza kuleta mabadiliko.”

Mkutano huu unafuatia miezi ya majadiliano ya serikali mbalimbali mjini New York ambayo yamezaa makubaliano kuhusu Tamko la Kisiasa la Doha, linalotarajiwa kupitishwa rasmi katika kikao cha ufunguzi.

Tamko hilo ndilo kitovu cha mkutano huu, amesisitiza Alya Ahmed Saif Al-Thani, Mwakilishi wa Kudumu wa Qatar katika Umoja wa Mataifa.

Amesema: “Ni wito wa kimataifa wa kuchukua hatua, unaozitaka serikali kujitolea tena kuunda mazingira bora ya kiuchumi, kisiasa, kijamii, kitamaduni na kisheria ili kufanikisha maendeleo ya kijamii kwa wote.”

Mabango katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa yakionesha Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs (Pichaya maktaba)

UN News/Abdelmonem Makki

Mabango katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa yakionesha Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs (Pichaya maktaba)

Wakati wa maamuzi muhimu

Ikiwa imesalia miaka mitano tu kufikia ukomo wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ifikapo mwaka 2030, dunia inasuasua katika maeneo mengi. Maendeleo katika kupunguza umaskini yamepungua kasi, usawa wa kijinsia umekwama, na vijana wengi wanakabiliwa na mustakabali usio na uhakika.

Mwaka jana, nchi wanachama zilipoomba kufanyika kwa mkutano huu, zilituma ujumbe ulio wazi: maendeleo ya kijamii lazima yarejee kuwa kiini cha ajenda ya kimataifa, ameeleza Bi. Sandkjær.

Ni kuhusu kujitolea tena kwa kiini cha Ajenda ya 2030 — kuhakikisha hakuna mtu anayeachwa nyuma.

Shughuli shirikishi na zenye mwelekeo wa mbele

Pamoja na vikao rasmi, programu ya sambamba itatoa nafasi ya ushirikiano na ubunifu.

Jukwaa la Asasi za Kiraia, Jukwaa la Sekta Binafsi, na Ukumbi wa Majawabu vitaangazia ubunifu katika ajira, ulinzi wa kijamii, na ustahimilivu wa jamii. Mitandao ya vijana na wanasayansi pia itashiriki kikamilifu, ikiwakilisha roho ya ubunifu wa pamoja na uwajibikaji wa kijamii.

Jukwaa jipya lililopatiwa jina la Jukwaa la Majawabu la Doha kwa Maendeleo ya Kijamii, , litakalozinduliwa kwa ushirikiano kati ya Qatar na Ufaransa, litaangazia ahadi na ubunifu halisi — kuanzia mageuzi ya sera hadi ushirikiano unaokabiliana na umaskini, ajira na ujumuishaji.

“Doha kwa mara nyingine inasimama kama ishara ya mshikamano wa kimataifa — mahali ambapo ahadi zinachochea vitendo, ushirikiano unasukuma maendeleo, na maono ya pamoja ya dunia jumuishi, endelevu na yenye amani yanakuwa halisi,” amesema Balozi Al-Thani.

Vijana wanaharakati wa tabianchi huko Maldives wakipaza sauti zao wakihimiza hatua za kukuza mazingira zichukuliwe..

© UNICEF/Pun

Vijana wanaharakati wa tabianchi huko Maldives wakipaza sauti zao wakihimiza hatua za kukuza mazingira zichukuliwe..

Safari ya mzunguko kamili

Kwa Bi. Sandkjær, ambaye alihudhuria Mkutano wa Kwanza wa Dunia kuhusu Maendeleo ya Kijamii mjini Copenhagen mwaka 1995 akiwa mwanaharakati kijana, Doha inawakilisha mwendelezo na mabadiliko. Alikumbuka kwamba wakati huo kulikuwa na matumaini makubwa — imani kwamba ushirikiano wa kimataifa ungeendelea kuleta maendeleo.

“Vijana wa leo wanakabiliwa na changamoto ngumu zaidi — taarifa potofu, wasiwasi wa tabianchi, na ukosefu wa imani,” amesema. “Lakini ujumbe wangu kwao ni rahisi: ushiriki wenu ni muhimu. Paza sauti zenu, tengenezeni ushirikiano, lisukume jambo.”

Kutoka maneno hadi vitendo

Bi. Sandkjær amesisitiza kuwa mafanikio ya mkutano hayatapimwa kwa hotuba, bali kwa utekelezaji.

Akasema: “Kwa tamko thabiti na ushirikiano uliopo tayari, kipimo halisi ni kutafsiri ahadi hizi kuwa maboresho ya kweli katika maisha ya watu — ajira zenye heshima, ulinzi wa kijamii, na ujumuishaji. Hapo ndipo tutajua tumeweza.”

Habari za moja kwa moja kutoka Idhaa ya Umoja wa Mataifa

Kadri viongozi wa dunia wanavyokusanyika Doha, matarajio ni makubwa — na dharura ni halisi. Miaka 30 baada ya Copenhagen, jukumu linasalia lile lile: kujenga dunia ambapo maendeleo yanapimwa si kwa utajiri pekee, bali kwa ustawi, usawa, na hadhi ya kibinadamu.

Idhaa ya Umoja wa Mataifa itakuwa ikiripoti moja kwa moja kutoka Doha wakati wote wa mkutano, ikileta habari, mahojiano na mitazamo kutoka kwa viongozi wa dunia, wanaharakati vijana, asasi za kiraia na wabunifu wa mabadiliko.

Fuata taarifa zetu kupitia majukwaa ya kidijitali na mitandao ya kijamii kwa masasisho ya papo kwa papo na simulizi za kibinadamu kutoka katika mkutano huu muhimu wa maendeleo ya kijamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *