Idara ya Vyombo vya Habari ya Serikali ya Palestina imetangaza kwamba mabomu 20,000 ambayo hayajalipuka bado yamebaki katika eneo la Ukanda wa Gaza huko Palestina.

Taarifa iliyotolewa na idara hiyo imesema, mabomu na mada hizo za milipuko zimetawanyika kwenye vitongoji vya makazi ya raia vilivyoharibiwa, nyumba na mashamba, na hivyo kuwa tishio la moja kwa moja na hatari kwa maisha ya raia, hasa watoto, wafanyakazi na wakulima wanaopita kwenye vifusi au kujaribu kuhuisha mashamba yao.

Idara ya Vyombo vya Habari ya Serikali ya Palestina imesema, mabomu hayo yamepigwa marufuku chini ya sheria za kimataifa na yana mada zenye mlipuko mkubwa ambayo yanaweza kubaki kwa miaka mingi, na hivyo kuwa sawa na mabomu ya kulipuka wakati wowote.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, hali hii inatishia usalama wa umma na inazuia juhudi za kujenga upya na kuwarejesha raia kwenye makazi yao.

Idara hiyo imesema kuwa: “Hadi sasa, kumerikodiwa matukio na milipuko mingi iliyosababishwa na mabaki ya zana za kivita za Israel, na imesababisha kuuliwa shahidi na kujerahiwa raia kadhaa, haswa watoto.

Itakumbukwa kuwa siku chache zilizopita afisa wa taasisi ya Humanity and Inclusion alisema kazi ya kukusanya silaha ambazo hazijalipuka katika Ukanda wa Gaza inaweza kuchukua kipindi cha miaka 20 hadi 30, akilitaja eneo hilo kama “uwanja wazi wa mabomu.”

Nick Orr, mtaalamu wa kukusanya silaha za milipuko katika shirika hilo, amefananisha hali ya sasa ya Gaza na ile iliyoshuhudiwa katika miji ya Uingereza baada ya Vita vya Pili vya Dunia.

Hifadhidata ya Umoja wa Mataifa imeonyesha kuwa zaidi ya watu 53 wameuawa na mamia kujeruhiwa kutokana na mabaki ya vita vya miaka miwili vya kuangamiza watu vilivyoanzishwa na Israel huko Gaza, huku mashirika ya misaada ya kibinadamu yakiamini kwamba idadi halisi inaweza kuwa kubwa zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *