Iran imesisitiza udharura wa kuendelea kuunga mkono uhuru, umoja wa ardhi na mamlaka ya kujitawala nchi ya Sudan huku vurugu kubwa zikiendelea kulitikisa taifa hilo la Afrika.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi alitoa matamshi hayo jana Ijumaa kwa mwenzake wa Sudan, Mohiuddin Salem katika mazungumzo ya simu ya wawili hao.

Araqchi ameelezea wasiwasi wake hasa kuhusu mashambulizi na mauaji ya raia katika mji wa la El Fasher kusini-magharibi mwa Sudan.

Mji huo umekuwa kitovu kipya cha wasiwasi wa kimataifa huku kukiwa na ongezeko kubwa la mzozo wa muda mrefu wa Sudan.

Jumanne wiki hii Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei alieleza kutiwa wasiwasi na mapigano ya silaha nchini Sudan hasa katika mji w El Fasher na kulaani “uharibifu wa miundombinu na mauaji ya watu wasio na hatia” katika mji huo ulioathiriwa na vita.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia ameonya kuhusu “harakati hatari zinazolenga kuigawanya tena Sudan,” na kusisitiza kuwa ipo haja ya kuheshimiwa mamlaka ya kitaifa na umoja wa ardhi ya nchi hiyo.

Baada ya kuzingirwa kwa miezi 18 mji wa El Fasher wenye raia karibu milioni 1.2, mji huo ambao ulikuwa ngome ya mwisho ya Kikosi cha Jeshi la Sudan (SAF) ulidhibitiwa kikamilifu na waasi wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *