Msemaji wa harakati ya Hamas amekosoa kauli za Kansela wa Ujerumani Friedrich Mertz za kujaribu kutetea uhalifu na jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya watu wa Palestina.

Msemaji wa Hamas amekosoa kauli za Kansela wa Ujerumani zinazohalalisha ukatili wa utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza na kumtaka Friedrich Merz ajiunge na jamii ya kimataifa katika kulaani utawala huo vamizi.

Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, Friedrich Merz alisema kwamba Ujerumani daima itaendelea kusimama na Israel, na sambamba na kufumbuia macho uhalifu na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni huko Gaza ameituhumu Hamas kuwa ndiyo sababu ya matatizo ya raia katika eneo hilo. Merz pia alisema Israel ni kimbilio la mamilioni ya Wayahudi na kusisitiza kwamba Berlin daima itasimama pamoja na Israel.

Matamshi ya Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz yametolewa wakati ambapo, licha ya kutangazwa usitishaji mapigano katika vita vya Gaza, utawala wa Kizayuni wa Israel unaendelea kufanya mashambulizi dhidi ya Wapalestina, na utawala huo unapuuza sheria za kimataifa na matakwa ya walimwengu, kwa kuendelea kuwaua shahidi au kuwajeruhi Wapalestina wengi wanaoishi Gaza. Zaidi ya hayo ni kwamba, licha ya hali mbaya ya inayoshuhudiwa huko Gaza hata katika kipindi cha sasa cha baada ya kusitisha mapigano, Israel inaendelea kuzuia juhudi za kuingia chakula cha kutosha na misaada ya kimatibabu katika eneo hilo, na hivyo kuendeleza hali mbaya na mateso kwa raia wa eneo hilo la Palestina.

Friedrich Merz, Kansela wa Ujerumani 

Katika hali hii, matamshi na msimamo wa Kansela wa Ujerumani akiiunga mkono Israel, kwa mara nyingine tena yamefichua ufa mkubwa uliopo kati ya kaulimbiu za nchi za Magharibi na sera zao za utendaji. Sisitizo la Friedrich Merz kwamba Ujerumani daima itaendelea kusimama na Israel na kupuuza kwake uhalifu na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni huko Gaza ni ushahidi dhahiri wa ukweli huu. Matamshi haya ya Kansela wa Ujerumani yametafsiriwa na Hamas na vilevile Rais wa Uturuki kuwa ni idhini isiyo ya moja kwa moja ya mauaji ya kimbari huko Gaza.

Matamshi ya Merz yanaonyesha mienendo inayokinzana ya nchi za Magharibi, hasa Ujerumani, katika siasa za kimataifa. Kwa upande mmoja, nchi hizo zinaitetea na kuikingia kufua Israel bila kikomo wala mpaka, na kwa upande mwingine, zinadai kutetea dhamiri ya binadamu na haki za mataifa yaliyokandamizwa! Nchi hizo zinaendelea kuusaidia kisiasa, kifedha na kwa zana za kivita utawala unaoua watoto huku taasisi na mashirika mengi ya kimataifa yakithibitisha katika ripoti zao rasmi kwamba utawala huo wa Israel unafanya mauaji ya kimbari huko Gaza. Kwa hakika, matamshi ya Kansela wa Ujerumani hayawezi kutambuliwa kama msimamo wa kidiplomasia tu; badala yake, yanapaswa kuonekana kama sehemu ya sera pana ya Magharibi, hasa Marekani, inayoukingia kifua na kuitetea Israel kwa hali na mali na kupuuza matakwa ya jamii ya kimataifa. Mkanganyiko huu wa nara na mienendo ya nchi za Magharibi unaibua alama ya kuuliza kuhusu uhalali wa kimaadili wa nchi za Magharibi, lakini pia kutayarisha mazingira ya kutokea mpasuko mkubwa zaidi katika mahusiano ya kimataifa.

Kwa miongo kadhaa, nchi za Magharibi, hasa Ujerumani, zimekuwa zikidai kutetea haki za binadamu na zinajiona kama waanzilishi wa kanuni za haki za binadamu na utawala wa sheria. Hii ni licha ya kwamba, kinyume na kaulimbiu na madai hayo yote, zinaendelea kuwa kimya mbele ya uhalifu wa wazi unaofanywa dhidi ya mataifa mengine au zimewaunga mkono rasmi wahalifu hao; mfano wa wazi ukiwa msimamo wa nchi hizo kuhusu mashambulizi ya Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza.

Hii leo maoni ya umma duniani yanaona waziwazi mkanganyiko uliopo kati ya madai ya haki za binadamu ya Magharibi na utendaji wao halisi.

Mwishowe, inatupasa kusema kuwa kinachojitokeza katika mzozo huu wa kidiplomasia kati ya Uturuki na Hamas kwa upande mmoja na Ujerumani katika upande mwingine ni kielelezo cha mgogoro wa kimaadili wa serikali za nchi Magharibi. Inaonekana kwamba, wakati umefika kwa wanasiasa wa Magharibi kusikiliza sauti ya dhamiri ya kimataifa inayolilia haki na ubinadamu, uhuru na uadilifu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *