Leo ni Jumamosi 10 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1447 Hijria ambayo inasadifiana na Mosi Novemba 2025 Miladia.

Katika siku kama ya leo miaka 122 iliyopita, Theodor Mommsen, mmoja wa waandishhi na wanahistoria wakubwa wa karne ya 19 nchini Ujerumani aliaga dunia. Alizaliwa 1819 nchini Ujerumani na katika kipindi cha umri wake aliandika, vitabu na makala 900 lakini kitabu chake muhimu zaidi ni The History of Rome. Mwaka 1902 Theodor Mommsen alitunukiwa tuzo ya nobel katika uga wa fasihi.

Theodor Mommsen

Miaka 111 iliyopita katika siku kama ya leo, serikali ya wakati huo ya Iran ilitangaza kutofungamana na upande wowote katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Hata hivyo udhaifu wa kisiasa wa watawala wa wakati huo, matatizo ya ndani, matatizo ya kivita na kupenda kujitanua kwa nchi zilizokuwa zikipigana katika vita hivyo ni mambo yaliyopelekea nchi hii kwenda kinyume na ahadi yake ya kutofungamana na upande wowote katika vita hivyo. Ni kutokana na hali hiyo, ndipo Iran ikajikuta katika hujuma na mashambulizi ya majeshi ya Uingereza, Urusi ya zamani na jeshi la Othmania na kuisababishia hasara kubwa.

Miaka 107 iliyopita katika siku kama ya leo ufalme wa Austria na Hungary ulisambaratika kufuatia kushindwa kwake katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Ufalme huo ambao ulikuwa umeundwa katika nusu ya pili ya karne ya 19, ulikuwa utawala mkubwa, wenye nguvu barani Ulaya na uliokuwa umepanua mamlaka yake kabla ya Vita vya Kwanza vya Dunia. Hata hivyo baada yya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia, tawala zilizoshinda vita hivyo, viliuugawa ufalme wa Aaaustia na Hungary katika nchi tatu za Austria, Hungary na Czechoslovakia kama fidia ya kushindwa.

Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita utawala wa kifalme nchini Uturuki ulihitimishwa rasmi na Kemal Ataturk. Baada ya kumalizika kwa Vita vya Kwanza vya Dunia sanjari na kudhoofika na kupoteza ushawishi wa utawala wa Othmania, Atatürk aliamua kuvunja utawala huo wa kifalme na kutwa uongozi. Hata hivyo haikuwa rahisi kwa Mustafa Kemal Atatürk kumaliza utawala wa kifalme wa Othmania ambao ulikuwa na misingi ya kidini. Hivyo mwanzoni alitenganisha baina ya utawala wa kisultani na cheo cha ukhalifa wa Waislamu na tarehe Mosi mwaka 1922 akavunja rasmi utawala wa kifalme huku cheo cha ukhalifa kikibakia kama cheo cha heshima tu. Suala hilo liliharakisha kuporomoka kwa utawala wa kifalme wa Othmania uliodumu kwa kipindi cha miaka 600. Baada ya kuporomoka utawala huo, uliundwa utawala wa Jamhuri na wa kisekulari hapo tarehe 29 Oktoba mwaka 1923. 

Katika siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, vilianza vita vya ukombozi wa Algeria baada ya kuundwa Harakati ya Ukombozi wa Algeria chini ya uongozi wa Ahmed ben Bella. Baada ya kupita miaka 132 ya utawala wa kikoloni wa Ufaransa nchini Algeria, hatimaye mwaka 1962 mapambano ya ukombozi ya wananchi Waislamu wa Algeria yalizaa matunda na nchi hiyo kujipatia uhuru wake. Baada ya kutangazwa uhuru wa Algeria, Ahmed ben Bella alikuwa rais wa kwanza wa nchi hiyo. Utawala wa Ahmed ben Bella ulidumu kwa miaka mitatu tu, kwani ulipofika 1965 alipinduliwa na Kanali Houari Boumediene aliyekuwa waziri wake wa ulinzi.    

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *