Vurugu zinazoendelea nchini Tanzania kufuatia Uchaguzi Mkuu wa 29 Oktoba 2025, zinatatiza usafirishaji wa bidhaa zinazopelekwa Rwanda, huku madereva wa malori wakieleza kuhusu kupotea kwa mawasiliano, uhaba wa mafuta na kukawia sana katika barabara kuu.
Nchi hiyo ya Tanzania ambayo ni jirani ya Rwanda imekumbwa na vurugu tangu 29 Oktoba 2025, siku ya Uchaguzi Mkuu, huku baadhi ya wananchi wakiingia mitaani kupinga matokeo ya awali ya uchaguzi wa urais ambayo yalimrejesha madarakani Samia Suluhu.
Maandamano hayo yameathiri baadhi ya huduma, ikiwemo malori yanayosafirisha bidhaa kupitia mpakani.
Inayohusiana
Katibu Mkuu wa Umoja wa Madereva wa Malori wa Rwanda, Noel Nkurikiye, aliambia New Times Rwanda, chombo vya habari nchini humo, kuwa hali inazidi kuwa mbaya kutokana na vurugu kuenea katika mikoa mikubwa ya Tanzania.
“Hakuna mawasiliano,” alisema.
“Madereva kwa kawaida huwasiliana na waajiri wao kwa ajili ya uratibu, hasa wanapohitaji kujaza mafuta, lakini hilo haliwezekani tena. Wengi wao waliishiwa na mafuta na kulazimika kusimama pale walipokuwa.”
Alisema vurugu hizo zilizoanzia miji ya Dar es Salaam na Dodoma, sasa zimefika eneo la Kahama karibu na Rwanda, na kuwalazimisha madereva wa mizigo kutoka Rwanda kusimamisha au kubadilisha njia.
“Katika siku za mwanzo za maandamano, malori yangeweza kusafiri hadi kufika maeneo ambayo hayakuwa salama tena. Sasa yamekwama katika maeneo ambayo sio mbali sana na mpaka.”