Katika matokeo ya hivi karibuni ya kashfa ya Jeffrey Epstein, Kasri ya Mfalme wa Uingereza, Buckingham Palace, ilitangaza jana Ijumaa kwamba Andrew, kaka wa mfalme wa Uingereza, atajulikana kama Andrew Mountbatten Windsor na si Mwanamfalme, na hatakuwa tena na haki ya kutumia vyeo vyake vyovyote vya kifalme.
Kasri ya Buckingham imetangaza kwamba Mwanamfalme Andrew atapoteza vyeo vyake vya kifalme na kuondoka katika makazi yake ya Royal Lodge huko Windsor.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa: Mfalme Charles ameanza “mchakato rasmi wa kufuta vyeo na heshima zote za Prince Andrew” na sasa atajulikana kama Andrew Mountbatten Windsor.

Uamuzi huo umechukuliwa huku familia ya kifalme ya Uingereza ikiwa na wasiwasi kuhusu kuchafuliwa sifa ya familia hiyo, wakati huu ambapo vichwa vya habari kuhusu urafiki wa Mwanamfalme Andrew na mnyanyasaji wa watoto aliyekuwa mahabusu, Jeffrey Epstein, na madai ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya Virginia Giuffre, mmoja wa waathiriwa wa Epstein, yakiibua wasiwasi.
Uamuzi huu unakuja kufuatia mashinikizo makubwa ya umma dhidi ya taasisi ya kifalme ya Uingereza yaliyotaka kutimuliwa Mwanamfalme Andrew katikka makazi yake, Royal Lodge, baada ya kuacha kutumia jina la Duke wa York mapema mwezi huu kutokana na uhusiano wake na mfanyabiashara wa Marekani, Jeffrey Epstein, ambaye alipatikana amekufa gerezani mwaka wa 2019 kabla ya kusikilizwa kesi yake ya uhalifu wa ngono.
Katika mahojiano ya BBC Panorama ya Desemba 2019, Giuffre alielezea jinsi Jeffrey Epstein alivyompeleka kwa Prince Andrew wa Uingereza, kwa njia ya biashara haramu ya ngono, jambo ambalo lilibadilisha maoni ya umma dhidi ya mwanamfalme huyo. Baadaye mwanamke huyo alimshtaki Mwanamfalme Andrew katika mahakama ya kiraia ya New York. Kesi hiyo iliamuliwa mnamo Februari 2022; na Prince Andrew alimlipa Giuffre kiasi ambacho hakikufichuliwa cha pesa. Giuffre alifariki dunia kwa kujiua mwezi Aprili mwaka huu wa 2025.