
Mji wa Maroua ambao ni makao makuu ya jimbo la Kaskazini la Cameroon limesimamisha shughuli zote za kibiashara ikiwa ni kuitikia mwito wa kiongozi wa upinzani aliyetangaza mgomo wa biashara kwa watu wote.
Habari za mwito wa kiongozi huyo wa upinzani, Issa Tchiroma Bakary wa kufanyika mgomo wa kitaifa chini ya kaulimbiu ya “mji wa wafu” zimeenea haraka kama moto kwenye nyika wakati wa kiangazi.
Mfanyabiashara mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Hayatou amesema alipohojiwa kwamba: “Ni vigumu sana kwetu wafanyabiashara. Tumelazimika kuitikia mwito huo kwani tulitishiwa kwamba soko litachomwa moto, ndiyo maana tumefunga maduka yetu leo.” Mfanyabiashara mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Mouhamadou Blama naye ameunga mkono matamshi ya Hayatou na kusema: “Hii inatusababishia matatizo mengi, na ni kwa sababu hiyo ndio maana miji imegeuka kama ya watu. Hakuna wateja wala wanunuzi wanaokuja kufanya manunuzi.”
Hasara kubwa zaidi inawapata wauzaji wa matunda kwa sababu hawapati msaada wowote wakati wanapoona bidhaa zao zinaoza. Muuzaji wa matunda Mahamout amesema kuwa ameshindwa kuuza chochote kwa sababu soko lilikuwa limefungwa tangu asubuhi.
Wafanyabiashara kama Adboul Aziz wanasema wanaogopa kwa sababu hakuna usalama kabisa.
Amesema: “Kuna maduka zaidi ya 2,000 sokoni, lakini hatuna ulinzi, hatuna polisi, hatuna vikosi vya kulinda usalama wakati tuna mali zetu nyingi sokoni.”
Sekta nyingine muhimu pia zimefungwa nchini Cameroon zikiwemo za elimu huku vijana wengi wakisema hawaendi maskulini kwa sababu ya ukosefu wa usalama.
Mwanafunzi mmoja aliyejitamblisha kwa jina la Gringa Dieudonné amesema: “Tulitakiwa kuwa wanafunzi 50 darasani, lakini tulikuwemo 20 tu darasani, leo asubuhi, na hii ni kwa sababu mji umegeuka kuwa wa wafu. Kutoka nje ni vigumu.”