Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema Marekani inadai kwamba inataka kutatua matatizo ya Lebanon lakini nchi hiyo sio mpatanishi mwadilifu asiyependelea upande wowote na ni mshirika katika uhalifu na jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Sheikh Naeem Qassem amepongeza msimamo wa Rais wa Lebanon wa kutoa agizo kwa jeshi kukabiliana na uvamizi wa utawala wa Kizayuni wa Israel akiutaja kuwa ni wa kuwajibika na wa kutegemewa na kuongeza kuwa: Msimamo huo unapaswa kuimarishwa kwa umoja na mshikamano. Vilevile ameihimiza serikali ya Beirut kuandaa mpango wa kulisaidia jeshi la taifa ili liweze kukabiliana na adui Mzayuni.  

Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema: “Tutakomboa ardhi ya nchi yetu kwa umoja na mshikamano. Lengo la Muqawama na mapambano ni kukomboa ardhi, lakini lengo la adui Mzayuni ni kughusubu na kukalia ardhi yetu kwa mabavu.”

Amesisitiza udharura wa kuzidishwa mashinikizo ili kuulazimisha utawala ghasibu wa Israel utekeleze makubaliano ya kusitisha vita na kusema: Nguvu ya Lebanon ni ngome kubwa na imara na Muqawama ndio kielelezo cha nguvu hiyo na unapaswa kulindwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *