Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mahmoud Thabit Kombo, amekanusha madai ya matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji wanaopinga zoezi la Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha Al-Jazeera siku ya Ijumaa, Waziri Kombo amesema hadi sasa hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa vikosi vya usalama vimetumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji hao. Aidha, alibainisha kuwa serikali haina takwimu rasmi kuhusu idadi ya waliopoteza maisha.

Kauli ya Waziri Kombo imekuja wakati mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu yakiendelea kutaka uchunguzi huru kufanyika kuhusu matukio ya vurugu yaliyotokea baada ya uchaguzi huo.

Mapema jana Chama kikuu cha upinzani nchini humo CHADEMA ambacho kilisusi na uchaguzi huo kikidai mageuzi ya kimfumo kimesema kuwa takriban watu 700 wameuawa kufuatia maandamano hayo yaliogubikwa na ghasia madaia ambayo hayajathibitishwa.

Mkuu wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi nchini humo Jenerali Jacob Mkunda alijitokeza hadharani kukosoa maandamano yanayoendelea akiwaita waandamanaji hao wahalifu, na kuwaonya pia dhidi ya kuendelea kuandamana, akisema jeshi halitasita kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria iwapo hali ya vurugu na maandamano itaendelea.

Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa vikosi vya usalama nchini Tanzania, kujizuwia kutumia nguvu kupita kiasi, dhidi ya waandamanaji. Umoja huo pia umetaka uchunguzi huru ufanyike kuhusiana na ripoti za ghasia zinazohusiana na uchaguzi.

Msemaji wa ofisi ya haki za binaadamu ya Umoja huo Seif Magago ameuambia mkusanyiko wa wajumbe mjini Geneva kwamba waandamanaji wanapaswa kuachwa kuandamana kwa amani.

Serikali bado haijatoa maoni kuhusu idadi ya vifo lakini imesisitiza kuwa uchaguzi uliendeshwa kwa amani na uwazi.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, matokeo rasmi yanatajiwa kutangazwaa leo hukuu mhombea wa chama tawala CCM akitarajiwa kuibuka na ushindi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *