
Tume Huru ya Uchaguzi nchini Tanzania imemtangaza Samia Suluhu Hassan kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais ulifanyika Oktoba 29 kwa asilimia 98 ya kura.
Watanzania waliotimiza masharti ya kupiga kura Jumatano iliyopita walielekea kwenye vituo vya kupigia kura kwa ajili ya kumchagua rais, wabunge na madiwani katika uchaguzi uliosusiwa na chama kikuu cha upinzani, CHADEMA na kushirikisha vyama vingine vingi vya siasa.
Matokeo hayo yanammpa Samia Suluhu Hassan aliyechukua madaraka mwaka wa 2021 baada ya kifo cha mtangulizi wake, John Pombe Magufuli, muhula mwengine wa pili wa miaka mitano kuiongoza nchi hiyo ya Afrika Mashariki yenye watu milioni 68.
Uchaguzi wa mara hii wa Tanzania uligubikwa na maandaamano katika jiji la Dar es Salaam na miji mingine kadhaa wakati wa upigaji kura siku ya Jumatano, huku waandamanaji wakilalamikia kukamatwa baadhi ya viongozi wa upinzani na kuzuiliwa kushiriki katika uchaguzi wa rais mbali na madai ya ukandamizaji ya wakosoaji wa serikali.
Chama cha CHADEMA ambacho kimesusia uchaguzi huo kilidai kuwa mamia ya watu wameuawa katika ghasia zilizofuatia Uchaguzi Mkuu. Hata hivyo Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Tanzania, Thabit Kombo amekanusha madai hayo.
Vilevile Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema ripoti za kuaminika zilionyesha kuwa karibu watu 10 waliuawa katika maandamano yaliyofanyika kwenye miji mitatu, ikiwa ni makadirio ya kwanza ya umma ya vifo yaliyotolewa na shirika hilo la kimataifa.