Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelitaja tangazo la Marekani la kuanza tena majaribio ya silaha za nyuklia kuwa ni kitendo kisicho cha kuwajibika na tishio kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa.

Sayyid Abbas Araqchi amesema kwamba Marekani ndiyo wakala hatari zaidi wa kueneza silaha za nyuklia duniani na kuongeza kuwa: “Kwa kauli moja, dunia inapaswa kuiwajibisha Marekani kwa kueneza silaha hizo hatari.”

Araghchi ameikosoa Washington kwa kubadilisha jina la “Wizara ya Ulinzi” kuwa “Wizara ya Vita” na kuishutumu Marekani kuwa ni “mnyanyasaji mwenye silaha za nyuklia.”

“Mnyanyasaji huyu huyu anataka mpango wa nyuklia wa amani wa Iran uonekane kuwa ni hatari na kutishia kufanya mashambulizi zaidi dhidi ya vituo vya nyuklia vinavyokaguliliwa na Umoja wa Mataifa; vitendo hivi vyote ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa,” amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran.

Araqchi amesema: “Tangazo la Marekani la kuanza tena majaribio ya silaha za nyuklia ni kitendo cha kurudi nyuma na kisichowajibika na ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa.”

Sayyid Abbas Araqchi amesisitizia kuwa: “Dunia lazima, kwa kauli moja, iilazimishe Marekani kuwajibika kwa kanza tena kueneza silaha hizo hatari.”

Matamshi haya ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran yamekuja baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kuiagiza Wizara ya Vita ya nchi hiyo kuanza tena majaribio ya silaha za nyuklia; katika uamuzi ambao umewatia wasiwasi wapinzani wa silaha za maangamizi ya umati na wataalamu masuala ya usalama duniani.

Wakosoaji kwa upande wao wametahadharisha kuwa kuhuisha majaribio ya moja kwa moja ya silaha za nyuklia kutavuruga jitihada za miongo kadhaa kuzuia usambazaji wa silaha hizo na kuruhusu majaribio mtawalia ya kulipiza kisasi kote ulimwenguni, na hivyo kuathiri Mkataba Unaopiga Marufuku Majaribio ya Nyuklia (CTBT).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *