
Shambulio la anga lililofanywa na jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel limesababisha vifo vya watu wanne na kuwajeruhi wengine watatu kusini mwa Lebanon ukiwa ni mwendelezo wa mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na Tel Aviv ndani ya ardhi ya nchi hiyo, ambayo yanakiuka makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwishoni mwa Novemba 2024 kati ya Harakati ya Muqawama ya Hizbullah na utawala huo ghasibu.
Kwa mujibu wa mtandao wa televisheni ya al-Mayadeen mauaji hayo yamesababishwa na shambulio la ndege isiyo na rubani ya Israel iliyolenga gari moja katika kijiji cha Kafr Rumman siku ya Jumamosi.
“Mapema siku hiyohiyo, ndege nyingine isiyo na rubani ya Israel ilifanya shambulio la anga katika mji wa karibu wa Kafr Sir,” imeeleza ripoti hiyo ya al-Mayadeen.
Mashambulio hayo yametokea siku tatu baada ya wanajeshi wa utawala ghasibu wa Israel kufanya mashambulizi ya ardhini katika mkoa wa kusini wa Lebanon wa Nabatieh, mahali yalipotokea mashambulizi ya jana Jumamosi.
Uchokozi huo mbaya umefanywa huku utawala haramu wa kizayuni wa Israel ukiendelea kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa Novemba 27, 2024.
Mkataba huo ulikuja kufuatia operesheni nyingi zilizotekelezwa mfululizo na harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Lebanon, Hizbullah dhidi ya maeneo nyeti na ya kimkakati katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu…/