Mamlaka za Palestina katika Ukanda wa Ghaza zimetangaza kuwa utawala wa kizayuni wa Israel umeruhusu kuingizwa katika eneo hilo sehemu ndogo tu ya misaada ya kibinadamu kinyume na ilivyoafikiwa katika makubaliano ya usitishaji mapigano yanayosimamiwa na serikali ya Marekani, ambayo yalianza kutekelezwa mwezi uliopita.

Katika taarifa iliyotoa siku ya Jumamosi, Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Serikali ya Ghaza imesema, ni malori 3,203 tu ya kibiashara na ya misaada yameingiza bidhaa za chakula na vifaa katika eneo hilo kuanzia Oktoba 10 hadi 31.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa, hiyo ni wastani wa malori 145 ya misaada kwa siku, au asilimia 24 tu ya malori 600 ambayo yanapaswa kuingia Ghaza kila siku kama sehemu ya makubaliano hayo ya usitishaji vita.

“Tunalaani vikali vizuizi unavyoweka utawala ghasibu wa Israel vya kuzuia misaada na malori ya kibiashara na tunaubebesha dhima kamili ya hali mbaya ya kibinadamu na inayozidi kuharibika ambayo inawakabili zaidi ya watu milioni 2.4 katika Ukanda wa Ghaza,” imeeleza taarifa ya ofisi hiyo.

Japokuwa uingizaji misaada huko Ghaza umeongezeka tangu makubaliano ya kusitisha mapigano yalipoanza kutekelezwa, lakini Wapalestina wa sehemu zote za eneo hilo lililowekewa mzingiro na jeshi la kizayuni wanaendelea kukabiliwa na uhaba wa chakula, maji, dawa na vifaa vingine muhimu kutokana na mzingiro huo uliowekwa na utawala ghasibu wa Israel.

Familia nyingi za Wapalestina hazina makazi pia ya kutosha, kwa sababu nyumba zao na vitongoji vyao vimebomolewa kikamilifu na mashambulio ya kinyama yaliyofanywa kwa muda wa miaka miwili na jeshi la Israel dhidi ya Ghaza.

Wakati huohuo, Stéphane Dujarric, msemaji wa Katibu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitangaza siku ya Alkhamisi kwamba ofisi ya kibinadamu ya umoja huo imeripoti kuwa ukusanyaji wa misaada “umekuwa mdogo” kutokana na “ubadilishaji wa njia ulioamriwa na mamlaka ya Israel”.

Wakati huo huo, jeshi la utawala wa kizayuni limeendelea kufanya mashambulizi katika kila pembe ya Ghaza kinyume na makubaliano ya kusitisha mapigano.

Jana Jumamosi, ndege za kivita za jeshi la utawala huo haramu, mizinga na vifaru vyake vilishambulia maeneo yanayozunguka Khan Younis, kusini mwa Ghaza. Jeshi pia lilibomoa pia majengo ya makazi ya watu mashariki mwa kambi ya wakimbizi ya Jabalia kaskazini mwa eneo hilo…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *