
Katika mazungumzo ya simu na Waziri Mkuu wa Jamaica, ambaye pia ni Waziri wa Ulinzi na Waziri wa Ukuaji wa Uchumi na Uundaji wa Ajira, Andrew Holness, Katibu Mkuu alieleza masikitiko yake makubwa na kuwatakia faraja wale wote walioathirika. Alisisitiza umuhimu wa msaada wa kimataifa katika kusaidia taifa hilo la Karibiani kukabiliana na athari za kimbunga hicho.
“Katibu Mkuu amesisitiza kuwa msaada wa kimataifa ni muhimu sana wakati huu,” ameandika Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, katika taarifa iliyotolewa jiji New York, leo Jumapili Novemba 3.
Ili kuimarisha juhudi za kibinadamu, Mratibu wa Misaada ya Dharura wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher, ametenga dola milioni 4 za Marekani kutoka Mfuko wa Dharura wa Kati wa Umoja wa Mataifa (CERF). Fedha hizo zitaruhusu mashirika ya Umoja wa Mataifa na washirika wake kuongeza haraka misaada ya kuokoa maisha kwa jamii zilizoathiriwa zaidi na kimbunga hicho.
Umoja wa Mataifa unaendelea kufuatilia hali hiyo kwa karibu na uko tayari kusaidia wananchi wa Jamaica kadiri juhudi za uokoaji na ujenzi upya zinavyoendelea.