Mapema usiku wa Ijumaa, Kasri ya Buckingham ilitoa taarifa rasmi ikitangaza kwamba Mwanamfalme Andrew amevuliwa vyeo vyote vya kifalme, majukumu rasmi na fursa za heshima, uamuzi ambao Mfalme Charles III aliutaja kuwa “usioepukika” kwa ajili ya kuepusha taasisi ya ufalme kuzama kwenye wimbi la kutoaminika nchini Uingereza.

Lakini je, kutolewa mhanga mwanamfalme mmoja tu kutamaliza mgogoro wa uhalali wa taji la ufalme wa Uingereza, au ni mwanzo tu wa maswali magumu kuhusu kuendelea kubakia madarakani mfumo wa kifalme uliojengeka kwenye misingi ya damu na ukoo katika karne ya 21?

Habari za Mwanamfalme Andrew kuvuliwa cheo cha kifalme mapema Ijumaa usiku ulikuwa mjadala mkuu katika vyombo vya habari vya Uingereza.

Uamuzi wa Mfalme Charles III wa kuanzisha mchakato rasmi wa kumvua rasmi Andrew vyeo vya kifalme sio tu mwisho wa kashfa ya kimaadili bali ni mwanzo wa sura mpya ya siku zijazo za ufalme wa Uingereza. Taasisi ambayo katika miaka ya karibuni imekumbwa na kashfa chungu nzima za kimaadili, mashinikizo ya maoni ya umma, changamoto za kifedha na kudhoofika uhalali wake.

Taarifa kutoka Kasri ya Buckingham ilitumia maneno rasmi lakini yenye uchungu: “Andrew Mountbatten wa Windsor hatakuwa tena na vyeo vya kifalme, majukumu rasmi wala fursa za heshima.” Baada ya miongo kadhaa, Uingereza inashuhudia maamuzi ambayo yameifikisha familia ya kifalme katika hatua ya kihistoria ya kuchagua kati ya damu ya kifalme au kuendelea kubakia ufalme.

Gazeti la Times liliandika kwamba hatua hii ilikuwa “chaguo lisiloepukika” na sio kwa msingi wa maadili. Mfalme Charles alichukua hatua hii ili kuzuia utawala wa kifalme kuzama katika wimbi la kutoaminika. The Guardian pia ilielezea katika uhariri wake uamuzi huu kuwa “upasuaji wa kuzuia kifo cha mgonjwa.” Sauti za wachambuzi kwenye redio ya LBC zilizungumzia nukta moja ya pamoja: ‘Ufalme umelazimika kujilinda, hata kama ni kwa gharama ya kumtoa mhanga mmoja wa watu wake wa karibu zaidi.’

Kilichoonekana kuharakisha uamuzi wa mfalme sio tu kuendelea kwa tuhuma zilizopo, bali kutolewa kwa barua pepe mpya zinazoashiria uhusiano wa Andrew na Jeffrey Epstein, mbali na madai ya awali. Raia wa Uingereza walikasirishwa sana, ambapo uchunguzi mpya wa maoni ulionyesha kwamba imani ya umma kwa familia ya Windsor ilikuwa imefikia kiwango cha chini kabisa katika miongo kadhaa iliyopita. Kile kilichofanya tukio hili kuwa zaidi ya kesi ya mtu binafsi ni swali gumu zaidi kuhusu falsafa na umuhimu wa ufalme katika karne hii ya 21. Je, taasisi iliyoasisiwa kwenye misingi ya uzawa na ukoo inaweza kudumu katika jamii ya leo yenye thamani huria za kidemokrasia?

Mfalme Charles III

Kwenye mitandao ya kijamii, alama za reli kama vile #NotMyPrince na #ModernMonarchy ziliibuka na kusambazwa pakubwa katika mitandao hiyo. Lakini mara hii, sio kusifu “sera za ukisasa za ufalme”, bali kukejeli juhudi za “ufalme kutaka kujiokoa wenyewe”. Vyuo vya Uingereza pia viliingia uwanjani. Wachambuzi wa Chatham House walisisitiza kuwa uamuzi huo ulikuwa “jibu la ufalme kujitetea dhidi ya mmomonyoko wa kijamii”.

Uchunguzi wa maoi wa kribuni ni dalili tosha ya mgogoro wa uhalali wa kifalme nchini Uingereza. Uungaji mkono kwa taasisi hii umeshuka kutoka takriban asilimia 75 hadi karibu asilimia 59 katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Katika tabaka la vijana walio na umri wa chini ya miaka 30, adadi hii imefikia karibu asilimia 36. Jamii ambayo hapo awali iliona taji kama ishara ya utulivu sasa inasisitiza kuchaguliwa viongozi kuliko ilivyokuwa huko nyuma.

Kashfa ya kimaadili ya karibuni ya Andrew ndio imepelekea kuakisiwa tena orodha ndefu ya kashfa za kimaadili za familia ya kifalme ya Uingereza. Uhusiano wa Charles na Camilla katika kipindi cha ndoa yake na Diana, uhusiano wa familia ya kifalme na madikteta na wanasiasa wanaochukiwa zaidi duniani na nafasi ya kihistoria ya kifalme katika biashara ya watumwa ni baadhi ya kashfa kubwa zinazohusishwa na familia ya kifalme ya Uingereza.

Kufuatia hatua ya kuvuliwa Mwanamfalme Andrew vyeo vyake vya kifalme, Charles III na William sasa wanakabiliwa na mtihani ambao si wa kisiasa tu bali wa kuainisha uwepo wao. Kumvua Andrew cheo chake cha kifalme bila shaka ni hatua muhimu ya kinembo, lakini swali linabakia pale pale: Je, nembo hii inaweza kutatua changamoto za mgawanyiko wa kiuchumi, dhulma ya kurithiwa na mgogoro wa uaminifu wa umma?

Ni wazi kwamba kuvuliwa anwani na vyeo vya Andrew kunaonyesha mwanzo wa enzi ya kuulizwa maswali magumu kuhusiana na uwepo wa mfumo mzima wa ufalme nchini Uingereza.  Je, mfumo wa kisiasa ambao mali na mamlaka huhamishwa kwa kuzingatia uzawa wa kiukoo bado unaweza kudai uhalali katika jamii ya kisasa? Andrew ni dalili moja tu, tatizo ni kubwa zaidi. Swali kuu sasa sio kile kilichomfika Andrew, bali ni nini kitaufika ufalme katika siku zijazo?Ufalme wa Uingereza unaweza kuvuka mzozo huu kwa sasa, lakini bila shaka hautakuwa tena mfumo sawa na wa huko nyuma. Kila hatua itakayochukuliwa kwa ajili ya kuulinda itakabiliwa na nyingine ya kuibadilisha au kuufutilia mbali kabisa. Hatau hizi hatimaye zitapelekea kuulizwa swali jingine muhimu kuwa je, taji bado ni suala la kutegemewa au lenyewe ni mzigo kwa taifa?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *