
Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Nishati ya Nyuklia (IAEA) amethibitisha tena kuwa, kwa mujibu wa ukaguzi wa moja kwa moja, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia.
Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, ameliambia shirika la habari la Rudaw kwamba: “Naweza kusema kuwa hakuna mpango wa silaha za nyuklia kwa sababu tumekuwa tukifanya ukaguzi. Tukiacha kukagua, tukikosekana, basi bila shaka mashaka huanza kuibuka.”
Kauli hii imetolewa wakati ambapo Iran ilionya kuwa utekelezaji wa kile kinachoitwa utaratibu wa “snapback” na urejeshaji wa vikwazo vya Umoja wa Mataifa na mataifa matatu ya Ulaya utabatilisha makubaliano yake na IAEA kuhusu kuanza tena ushirikiano, makubaliano yaliyotiwa saini mjini Cairo tarehe 9 Septemba.
Hatua hiyo ilifuatia uamuzi wa Bunge la Iran kupitisha kwa kauli moja sheria inayoitaka serikali kusitisha ushirikiano wote na IAEA kufuatia mashambulizi ya pamoja ya Israel na Marekani mwezi Juni, yaliyolenga vituo vitatu vya nyuklia vya Iran kwa njia inayokiuka wazi sheria za kimataifa na Mkataba wa Kuzuia Ueneaji wa Silaha za Nyuklia (NPT).
Grossi amekiri kuwepo kwa hofu za kiusalama kutoka upande wa Iran, akisema kuwa kama kiongozi wa IAEA, “juhudi yangu ni kuendeleza mchakato wa kidiplomasia ili kuelewa hofu zao kutokana na kushambuliwa. Kwa hivyo wana wasiwasi, na tunataka kuyashughulikia.”
Kwa mujibu wa sheria ya Bunge, wakaguzi wa IAEA hawataruhusiwa kuingia Iran kama hakuttakuwa na uhakikisho wa usalama wa vituo vya nyuklia vya nchi na shughuli zake za amani za nyuklia.
Sababu kuu ya hatua hiyo ni azimio la IAEA ambalo lilikuwa msukumo wa kisiasa uliofungua njia kwa mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran mwezi Juni. IAEA haikulaani mashambulio hayo ya kigaidi ambayo yaliwalenga rais, wanasayanis wa nyuklia, makamanda wa kijeshi na vituo vya nyuklia.
Kuhusu picha za setilaiti zinazodai kuonyesha harakati katika baadhi ya vituo vya nyuklia vya Iran, Grossi alisema kuwa hizo ni “harakati za kawaida.”