Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa pongezi za dhati kwa Rais na watu wa Algeria kwa mnasaba wa maadhimisho ya miaka 71 ya kuanza Mapinduzi ya Ukombozi na Siku ya Taifa ya Algeria na kusema: Uhusiano wa kihistoria kati ya Iran na Algeria unafungua njia ya kupanuliwa zaidi uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Katika ujumbe wake kwa Abdelmadjid Tebboune na watu wa Algeria Rais Masoud Pezeshkian amesema: “Nina imani kwamba kwa kuzingatia uhusiano wa kihistoria na mambo yanayofanana kati ya nchi hizo mbili na kwa kutumia uwezo uliopo, tutashuhudia upanuzi zaidi wa uhusiano kwa mujibu wa maslahi na manufaa ya mataifa haya mawili.”
Ameongeza kuwa: “Moyo wa kupinga ukoloni, kupigania uhuru na ushujaa wa watu na viongozi wa Algeria katika miongo kadhaa ya mapambano ya uhuru dhidi ya ukoloni, umekuwa chanzo cha msukumo kwa mataifa na viongozi na wapigania uhuru kote duniani.”
Ufaransa iliikoloni Algeria kwa miaka 132 na hatimaye nchi hiyo ilipata uhuru mwaka 1962 baada ya miaka mingi ya mapambano ya ukombozi ya umwagaji damu.
Wanajeshi wa Ufaransa walipora maliasili za Algeria baada ya kuikoloni nchi hiyo kwa miaka mingi na kutekeleza jinai chungu nzima dhidi ya watu wa nchi hiyo. Algeria ilikoloniwa na Ufaransa kwa miaka 123.

Zaidi ya Waalgeria milioni moja waliuliwa na wanajeshi wa Ufaransa katika kipindi cha vita vya kupigania ukombozi wa Algeria kuanzia mwaka 1954 hadi 1962.