
Rais Donald Trump wa Marekani ametishia kufanya mashambulizi ya kijeshi ndani ya ardhi ya Nigeria kutoa mjibizo kwa alichodai kuwa ni ukatili wanaofanyiwa Wakristo, akisema ameiagiza Wizara yake ya Vita aliyoipa jina hilo jipya hivi karibuni “kujiandaa kwa hatua zinazowezekana” kuchukuliwa.
Katika ujumbe alioweka kwenye mtandao wa kijamii, Trump amesema Marekani itakata mara moja misaada yote kwa nchi hiyo ya Afrika “ikiwa Serikali ya Nigeria itaendelea kuruhusu mauaji dhidi ya Wakristo”.
Ameendelea kueleza kwamba Washington itachukua hatua ya kuwafuta aliowaita magaidi wa Kiislamu wanaofanya ukatili huo wa kutisha, lakini pasi na kufafanua magaidi anaowakusudia wala aina ya ukatili wanaofanya dhidi ya Wakristo wa Nigeria.
Sehemu moja ya ujumbe huo wa rais wa Marekani inasema: “kwa hivyo ninaiagiza wizara yetu ya vita ijiandae kwa hatua zinazowezekana kuchukuliwa. Kama tutashambulia, litakuwa (shambulio) la kasi, kali, na tamu, kama vile majambazi wa kigaidi wanavyowashambulia Wakristo wetu WAPENDWA! ONYO: NI VYEMA SERIKALI YA NIGERIA ICHUKUE HATUA HARAKA!”
Katika miezi ya karibuni, wabunge wa mrengo wa kulia na shakhsia wengine mashuhuri nchini Marekani wamekuwa wakidai kwamba mizozo ya utumiaji nguvu inayotokea nchini Nigeria ni sehemu ya kampeni ya “mauaji ya kimbari ya Wakristo”.
Wakati makundi ya kutetea haki za binadamu yanaihimiza serikali ya Nigeria ichukue hatua madhubuti zaidi kushughulikia machafuko yanayotokea ndani ya nchi hiyo, ambayo inakumbwa na mashambulizi ya mauaji yanayofanywa na Boko Haram na makundi mengine yanayobeba silaha, wataalamu wanasema madai kwamba kinachotokea Nigeria ni “mauaji ya kimbari ya Wakristo” ni uwongo na hayana mashiko.
Wamesisitiza kuwa hujuma na mashambulio yanayofanywa na makundi yanayobeba silaha ndani ya Nigeria yanawalenga Wakristo, Waislamu na hata wafuasi wa dini za jadi.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria, Kimiebi Ebienfa, amesisitiza kuwa nchi yake imejifunga na jukumu la kuwalinda raia wake wote.
Ebienfa ameeleza katika taarifa: “Serikali ya Shirikisho ya Nigeria itaendelea kuwalinda raia wote, bila kujali rangi, imani, au dini (zao)”…/