Msemaji wa Umoja wa Mataifa ameangazia hatari zinazowakumba waandishi wa habari duniani kote, akielekeza macho hasa kwa Ukanda wa Gaza, ambapo ametaja eneo hilo la Palestina lililozingirwa na utawala wa Israel kuwa eneo hatari zaidi kwa waandishi wa habari hivi sasa dunaini.

Stephane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amewaambia waandishi wa habari kwamba: “Karibu asilimia tisini ya mauaji ya waandishi wa habari hayajapatiwa ufumbuzi. Gaza imekuwa eneo hatari zaidi kwa waandishi wa habari katika mizozo iliyopo.”

Dujarric amebaini kuwa Katibu Mkuu Antonio Guterres anatoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi “huru na usioegemea upande wowote” kuhusu mauaji ya waandishi wa habari, akisisitiza kuwa “kutowajibika ni shambulio dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari na tishio kwa demokrasia yenyewe.”

Kauli hizi zinakuja huku Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ikiripoti kuwa angalau waandishi wa habari 248 wamepoteza maisha yao huko Gaza tangu Oktoba 7, 2023 wakati utawala haramu wa Israel ulipoanzisha mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa eneo hilo.

Shirikisho la Mashirika ya Habari la Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) limeeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu mauaji ya mara kwa mara ya waandishi wa habari wa Kipalestina yanayotekelezwa na vikosi vya Israel.

Shirikisho hilo limesema matukio yanayoendelea Gaza ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa, yakifanyika sambamba na ukiukaji wa Israel dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari, pamoja na mbinu zake za kuficha ukweli, kunyamazisha upinzani, kuficha makosa ya kila siku, na kuzuia taarifa kufika kwa jumuiya ya kimataifa.

Kuhusu hali ya sasa katika Ukanda wa Gaza, Dujarric amesema kuwa juhudi za kibinadamu zinaendelea licha ya ripoti za mashambulizi mapya ya anga ya Israel dhidi ya eneo hilo lililozingirwa.

Aidha, Dujarric ameashiria kuendelea kwa kuporomoka kwa mfumo wa afya wa Gaza, ambao unashindwa kukidhi mahitaji makubwa ya wakazi wake.

Kwa mujibu wa Dujarric, kufikia Oktoba 7 mwaka huu, zaidi ya wahudumu wa afya 1,700 wamepoteza maisha katika mashambulizi ya Israel dhidi ya eneo hilo tangu Oktoba mwaka 2023.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *