
Maporomoko ya udongo yaliyoathiri maeneo ya magharibi mwa Kenya yameuwa watu wasiopungua 21 na kujeruhiwa makumi ya wengine. Watu wengine zaidi ya 30 hawajulikani walipo kufuatia maafa hayo.
Maporomoko hayo ya udongo yalitokea mapema jana katika eneo bunge la Marakwet ambalo linapitia msimu wa mvua.
Kipchumba Murkomen Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya amesema kuwa hadi sasa wamethibitisha kuaga dunia watu 21 katika maafa hayo na wengine zaidi ya 30 hawajulikani walipo hadi sasa kama ilivyoripotiwa na familia zao.
Wakati huo huo, watu 25 waliojeruhiwa vibaya katika maporomoko ya udongo Kenya walifikishwa hospitali kwa jaili ya matibabu huko Eldoret huku wale wenye majeraha madogo walitibiwa katika hospitali za mashinani.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya amesema zoezi la kuwasaka waathirika na uokozi litaanza tena leo Jumapili.
” Tunafanya kazi kwa udharura wa kuratibu juhudi za uokoaji, kupanua usaidizi wa kibinadamu, na kuwa bega kwa begaa na familia zilizoathiriwa na maafa ya maporomoko ya ardhi huko Marakwet Mashariki,”amesema Kipchumba Murkomen.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya pia amewataka watu wanaoshi karibu na mito ya msimu au katika maeneo ambayo maporomoko ya ardhi yalitokea jana usiku kuelekea atika maeneo salama.