
Ligi ya mabingwa barani Ulaya inaendelea wiki hii kwa michezo kadhaa ya kusisimua.
Mabingwa wa Ligi Kuu ya kandanda ya Ujerumani Bayern Munich, watakuwa na kibarua kigumu siku ya Jumanne watakapomenyana na mabingwa watetezi Paris Saint-Germain.
Bayern Munich wameanza msimu huu kwa kishindo, wameshinda mechi 15 kati ya 15 katika mashindano yote hadi sasa msimu huu, na kuweka rekodi mpya ya mwanzo mzuri zaidi katika ligi tano bora za Ulaya.
Mwanzo huo mpya umeongeza matumaini kwa timu hiyo yaBavaria kwamba inaweza kulipambania kombe la UEFA msimu huu. Hata hivyo mtihani mkubwa utakuwa dhidi ya mabingwa watetezi PSG tena wakiwa nyumbani kutatoa taswira ya halisi ya uwezo wa Bayern katika safari yao ya kutwaa mataji msimu huu.
Kocha wa Bayern Munich Vincent Kompany amekuwa na wakati mzuri na kikosi hicho kitamtegemea nyota Harry Kane.
Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Uingereza amefunga mabao 22 katika michezo 15 katika mashindano yote, huku mchango wake wa ubunifu uwanjani ukitajwa kuwa muhimu sana.