
Awamu mpya ya maandamano ya baada ya uchaguzi inaanza leo Jumatatu, Novemba 3, 2025, katika miji kote nchini Cameroon. Issa Tchiroma Bakary,aliyechukuwa nafasi ya pili katika uchaguzi wa urais, ambaye amekataa matokeo ya uchaguzi, anaitisha maandamano ya siku tatu, akiwataka raia “kususia shughuli za serikali”. Hii ina maana, kwa nadharia, kwamba kila shughuli lazima isitishwe: ofisi za serikali, biashara, shule, na usafiri wa umma.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Na mwandishi wetu maalum huko Douala, Polycarpe Essomba
Huko Douala, mji mkuu wa kiuchumi wa nchi hiyo na kitovu cha maandamano ya wiki iliyopita pamoja na Garoua, kaskazini mwa Cameroon, hali hiyo itafuatiliwa kwa karibu tena, haswa ili kutathmini kiwango cha uungwaji mkono kwa wito huu wa kusitisha shughuli zote.
Christian anauza bidhaa mbali mbali dukani katika eneo la Carrefour Conquête, kama mita mia mbili kutoka hospitali kuu ya jiji la Douala. Leo Jumatatu, Novemba 3, 2025, ameamua: hatafungua. “Sifungui kwa usalama wangu mwenyewe, na pia kwa sababu ya mvutano kati ya pande hizo mbili. Nitakaa nyumbani na kufuatilia kwa wiki moja,” anaeleza.
Duka la William liko katika wilaya ya Akwa, katika kituo cha biashara. Kama Christian, atafunga leo Jumatatu, lakini si kama anaunga mkono agizo la “kusitishwa kwa shughuli zote”, ni kwa hofu tu.
“Wito wa kustishwa kwa shughuli zote nchini umetolewa. Wakati huo huo, mamlaka haitupi dhamana yoyote. Kwa hivyo, tumeamua kufuata mwongozo wa wengi, ambao ni kufunga biashara. Ninaunga mkono walio wengi: kaa nyumbani, funga duka, hadi taarifa zaidi itakapotolewa,” anaeleza.
Hofu ya hali ngumu
Geremy, mwenye umri wa miaka hamsini, ana wasiwasi kuhusu machafuko ambayo jiji linaweza kupitia. Analalamika kuhusu uharibifu wa barabara, vituo vya mafuta vilivyoharibiwa, na magari mengi yaliyochomwa moto. “Vitendo viovu havikaribishwi wakati wa maandamano au unapotetea madai yako. Kuandamana kwa kuonysa madai yako ni jambo moja, na hasira ni jambo lingine ambalo ni tofauti na hilo la kwanza, lakini ni makosa kuharibu,” anasema. “Huu ni uwekezaji unaofutwa, unaoharibiwa, na ni juhudi za raia wenzetu. Inasikitisha kwamba matairi yanawekwa barabarani na kwamba uwekezaji wenye thamani ya mabilioni unaweza kupotea kwa njia hii.” “
Makovu bado yanaonekana wazi hapa na pale jijini, na kulazimisha baadhi ya watu kuhifadhi vifaa kwa ajili ya familia zao huku wakisubiri kuona jinsi mambo yatakavyokuwa mwishoni mwa wiki.
Kwa upande wake, serikali imelaani “wito wa kusitisha shughuli zote,” ambao imesema ” hali hiyo inaweza kuhatarisha maisha ya taifa.” Waziri wa Mawasiliano, René Emmanuel Sadi, msemaji wa serikali, amewataka wote waliohusika katika uchaguzi wa urais kukubali matokeo yaliyotangazwa. Amesisitiza kwamba serikali imechukua hatua za kurejesha utulivu. Waandamanaji wanaofanya vitendo vikali vya vurugu wataadhibiwa kwa mjib wa sheria. Waziri wa Mawasiliano pia amesifu “ujasiri na uzoefu wa vikosi vya usalama” kabla ya kukosoa misimamo iliyochukuliwa na nchi rafiki za Cameroon na washirika wa kimataifa kuhusu mgogoro wa baada ya uchaguzi.