
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema, mzozo uliopo kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Marekani ni wa “dhati halisi” na wala hautokani na kauli mbiu; na chimbuko lake liko kwenye mgongano wa kimsingi wa maslahi; na akaeleza bayana kwamba, suala la ushirikiano na Marekani linaweza kuja kufikiriwa siku za usoni na si sasa hivi wala katika muda wa karibu
ikiwa Washington itasitisha kikamilifu utoaji msukumo, misaada na uungaji mkono kwa utawala wa kizayuni wa wa Israel, ikiondoa kambi zake za kijeshi kutoka eneo hili, na kuacha kuingilia masuala ya Iran.
Ayatullah Khamenei, ameyasema hayo leo alipohutubia maelfu ya wanafunzi, wanachuo na familia za mashahidi wa Vita vya Siku 12 kwa mnasaba wa kuwadia tarehe 4 Novemba ya kuadhimisha “Siku ya Wanafunzi na Siku ya Taifa ya Kupambana na Uistikbari Duniani” ambayo inasadifiana na kumbukumbu ya kutekwa “Pango la Ujasusi” la uliokuwa ubalozi wa Marekani hapa mjini Tehran mnamo mwaka 1979 na akasisitiza kuwa, tukio hilo ni la kihistoria na linalobainisha utambulisho.
Amesema: “mzozo uliopo kati ya Jamhuri ya Kiislamu na Marekani ni wa dhati halisi, na ni wa mgongano wa maslahi kati ya pande mbili. Ni ikiwa tu Marekani itakomesha kikamilifu uungaji mkono wake kwa utawala uliolaaniwa wa Kizayuni, ikaondoa kambi zake za kijeshi katika eneo, na kuacha uingiliaji wake, ndipo ombi la Marekani la ushirikiano na Iran litazingatiwa—na si sasa hivi au katika siku za karibuni, bali ni hapo baadaye”.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amekuelezea kutekwa kwa ubalozi wa Marekani mwaka 1979 kuwa ni “siku ya fahari na ushindi” na kielelezo cha utambulisho halisi wa serikali ya Marekani.
Amesema: “kutekwa kwa ubalozi wa Marekani kulifichua utambulisho halisi wa serikali ya Marekani na dhati halisi ya Mapinduzi ya Kiislamu”.
Ayatullah Khamenei ameeleza kwamba chimbuko la mivutano kati ya Marekani na Iran linarejea kwenye mapinduzi ya kijeshi ya 1953 yaliyompindua Waziri Mkuu Mohammad Mossadegh. Amesema, Marekani ilikula njama na Uingereza kumuangusha Mossadegh licha ya kujionyesha hadharani kuwa inamuunga mkono.
“Wamarekani walionyesha tabasamu kwa Mossadegh, lakini kwa kisirisiri, kwa kushirikiana na Waingereza, waliandaa mapinduzi ya kijeshi, wakaipindua serikali ya kitaifa, na kumrudisha Shah aliyekuwa anatoroka (nchi)”, ameeleza Kiongozi wa Mapainduzi.
Ayatullah Khamenei ameitoa maanani pia hoja ya kudai kwamba, kauli mbiu za kuipinga Marekani kama kusema “Mauti kwa Marekani” ndizo zinazochochea uadui wa Washington dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Amefafanua kwa kusema: “suala la Marekani na Jamhuri ya Kiislamu ni la dhati halisi, ni mgongano wa maslahi, si kauli mbiu”.
Ayatullah Khamenei amekumbusha kuwa, kutekwa ubalozi wa Marekani 1979 hapo awali kulikusudiwa kudumu kwa siku chache tu kama nembo ya kuakisi hasira ya umma, lakini baadaye kulifichua njama kubwa zaidi ilizokuwa imepanga Marekani dhidi ya Mapinduzi na akasema: “wanachuo waligundua nyaraka zilizoonyesha kwamba, ubalozi huo ulikuwa kitovu cha njama dhidi ya Mapinduzi”.
Katika hotuba yake hiyo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amewahimiza pia wanafunzi kuongeza ujuzi na ufahamu wao kuhusu historia ya kisiasa ya Iran na changamoto za sasa, kuimarisha sayansi, na kudumisha maendeleo katika nguvu na uwezo wa kijeshi ili kuonyesha kuwa “Iran ni taifa imara ambalo hakuna dola linayoweza kulitiisha na kulipigisha magoti”…/