
Taarifa iliyotolewa The Hague, Uholanzi leo na ICC inasema, matukio hayo ni sehemu ya mfululizo wa vitendo vya ukatili ambavyo vimeendelea kuikumba eneo la Darfur tangu Aprili 2023.
Ofisi hiyo imesema kwamba iwapo madai hayo yatathibitishwa, yanaweza kuainishwa kama uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu chini ya Mkataba wa Roma ulioanzisha ICC.
ICC imekumbusha kwamba kwa mujibu wa Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 1593 la mwaka 2005, mahakama hiyo ina mamlaka ya kisheria kuchunguza uhalifu unaoendelea kufanywa katika mgogoro wa Darfur.
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka inaendelea na uchunguzi juu ya uhalifu unaodaiwa kufanywa tangu kuzuka kwa mapigano hayo mwaka 2023.
Katika taarifa yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ICC imesisitiza kuwa kazi inaendelea kwa kasi kupitia mikusanyiko ya ushahidi mashambani, mahusiano ya karibu na waathirika na asasi za kiraia, pamoja na ushirikiano ulioimarishwa na mamlaka za kitaifa na mashirika ya kimataifa.
Kuhusu matukio mapya El-Fasher, ofisi hiyo imesema inachukua hatua za haraka kukusanya na kuhifadhi ushahidi muhimu utakaotumika katika mashitaka yajayo.
Aidha, ICC imekumbusha hukumu ya hivi karibuni dhidi ya kiongozi wa wanamgambo wa Janjaweed, Ali Muhammad Ali Abd-Al-Rahman al maarufu Ali Kushayb, aliyehukumiwa kwa uhalifu uliofanywa Darfur mwaka 2004, kuwa ni onyo kwa wahusika wote wa vita vya Darfur kwamba hakutakuwa na msamaha kwa uhalifu wa aina hiyo.
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka imewataka watu binafsi na mashirika yanayohusiana na masuala ya haki na uwajibikaji kuwasilisha taarifa au ushahidi wowote unaohusiana na matukio ya hivi karibuni au ya awali huko El-Fasher kupitia mfumo salama wa mtandaoni wa OTP.
Imetamatisha kwa kusema kuwa “hakutakuwa na amani ya kweli bila haki. Wale wanaowajibika kwa uhalifu huu watapaswa kujibu mbele ya sheria.