Afisa wa zamani wa masuala ya kijasusi wa Marekani ambaye pia ni mkaguzi wa zamani wa Umoja wa Mataifa amesema kwamba Marekani haina mfumo wa ulinzi wa makombora unaoweza kukabiliana na shambulio la kombora la Burevestnik la Russia.

Scott Ritter ametangaza hayo hadharani katika mahojiano maalumu na shirika la habari la Novosti na kuongeza kwamba mfumo wa ulinzi wa Marekani hauwezi kukabiliana na kombora la Burevestnik la Russia kwa sababu ili kukabiliana na kombora hilo lazima Washington iunde mfumo tofauti kabisa wa ulinzi wa makombora ambao utabadilisha kabisa mifumo yake ya ulinzi kwa digrii 360 kwa ajili ya kulinda maeneo ya Marekani lakini hivi sasa Washington haina uwezo wala vifaa vya kuunda mfumo wa namna hiyo.

Ritter pia amesema, kombora la Burevestnik lina uwezo wa kujibadilisha na kuruka kwa kasi kubwa na kukwepa mifumo ya kisasa ya ulinzi wa makombora iliyopo duniani leo.

Kwa upande wake, Rais Vladimir Putin wa Russia aliwahi kusema huko nyuma kwamba majaribio ya kombora la Burevestnik la masafa marefu yamefanyika kwa mafanikio.

Naye Mkuu wa Jeshi la Russia, Jenerali Valery Gerasimov amesema kuhusu kombora hilo kwamba, lina uwezo mkubwa wa kukwepa mifumo ya ulinzi wa makombora na pia kupambana na ndege za kivita.

Jenerali Gerasimov pia amesema kuwa, wakati wa kufanyiwa majaribio, kombora hilo la Burevestnik lilipiga shabaha ya umbali wa 14,000 na limetengenezwa kwa ajili ya kupiga maeneo ya mbali zaidi ya hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *