Mnamo Oktoba 26, Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vya Jenerali Hemedti, ambavyo vinapigana na jeshi la Jenerali al-Burhan tangu Aprili 15, 2023, vilitwaa udhibiti wa mji mkuu wa Jimbo la Darfur Kaskazini magharibi mwa Sudan. Tangu wakati huo, ushuhuda kutoka kwa raia kuhusu unyanyasaji wa RSF umeendelea kutolewa.

Imechapishwa:

Dakika 3 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Siku ya Jumatatu, Novemba 3, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai imeonya kwamba ukatili unaofanywa huko El-Fasher “unaweza kuwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.”

Tangu kutekwa kwa mji wa El-Fasher, mji mkuu wa Darfur Kaskazini, na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) mnamo Oktoba 26, baada ya kuzingirwa kwa miezi 18, mji huo uko katika hali nzito, na hakuna mawasiliano yoyote ya simu baada ya kuzimwa mitambo ya mawasiliano. Ripoti za ukatili zinaendelea kutolewa.

Kulingana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM), takriban watu 70,000 wamefanikiwa kuondoka El-Fasher, wakiwemo 5,000 ambao wamefika Tawila, kilomita 60 kutoka mji huo. Lakini makumi ya maelfu bado wamenaswa katika jiji hilo, ambapo hali ni inayowakumba wakaazi wa mji huo ni “ya khuzunisha,” kama Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul alivyoelezea mwishoni mwa juma lililopita.

Mamia ya watu wanaojaribu kuondoka El-Fasher wanazuiliwa na Vikosi vya RSF, ambavyo hunyang’anya magari yao na kuwalazimisha kurudi jijini au kuwateka nyara. Mtandao wa Madaktari wa Sudan unaripoti kwamba maelfu ya watu wanashikiliwa na RSF. Baadhi wameachiliwa na wameshuhudia ukatili waliofanyiwa.

Hiki ni kisa cha mtu aliyeomba kutotajwa jina, aliyewasiliana na sshirika la habari la AFP. Anadai alikamatwa pamoja na watu wengine 200 katika kijiji kidogo cha Garni, karibu na El-Fasher, sehemu ya lazima ya usafiri kwa wakazi wanaokimbia jiji. Kundi hilo lilishikiliwa mateka katika shule ambapo wafungwa wapya walifika kila siku. Walipigwa, walitukanwa, na walipokea mlo mmoja tu kwa siku, anashuhudia.

Tangu Oktoba 26, ripoti za unyanyasaji zimeongezeka: mauaji ya kikatili, ubakaji, uporaji, na mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa wa mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu. Baadhi wanaripoti kodi zinazotozwa kwa ndugu wa wafungwa ili kuweza kuachiliwa kwao.

RSF kuorodeshwa kama kundi la kigaidi

Tangu kukamatwa kwa El-Fasher, mamlaka katika Port Sudan imekuwa ikishinikiza tena RSF iorodheshwe kama kundi la kigaidi. Serikali ya Sudan inazingatia ombi lake juu ya unyanyasaji unaoendelea kuripotiwa kutoka Darfur, anabainisha mwandishi wetu wa kikanda, Gaëlle Laleix. Katika taarifa iliyochapishwa mwisoni mwa juma hili lilopita, ubalozi wa Sudan nchini Ufaransa ulishutumu “mauaji dhidi ya raia […] pamoja na shughuli kubwa za utakaso wa kikabila” zinazofanywa na kile unachokiita “wanamgambo wa kigaidi.”

Ombi kutoka kwa mamlaka ya Port Sudan si jipya. Mapema mwaka wa 2023, mwanzoni mwa vita, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, kamanda wa jeshi la serikali, aliuomba Umoja wa Mataifa kutangaza RSF kama kundi la kigaidi.

Kwa mara ya kwanza, ombi hili limevutia umakini wa kimataifa. Siku ya Alhamisi, wanachama wa Kamati ya Mahusiano ya Kigeni ya Bunge la Seneti la Marekani waliiomba Wizara ya Mambo ya Nje ichunguze jambo hilo. “Shambulio lililotabiriwa kwa muda mrefu na RSF dhidi ya raia wa El-Fasher, kwa sababu ya kabila lao, linaonyesha wazi kwamba Marekani lazima izingatie kuitangaza RSF kama kundi la kigaidi,” taarifa yao inabainisha.

Uteuzi huu unahusisha vikwazo kama vile kuzuiwa kwa mali za viongozi wa kundi hilo katika nchi za kigeni na marufuku ya silaha. Mnamo mwezi Mei 2024, Wizara ya Fedha ya Marekani  iliwachukuliwa vikwazo viongozi wawili wa RSF kwa jukumu lao katika kuzingirwa kwa El-Fasher.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *