
Msemaji wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) ameashiria hali mbaya inayowakabili zaidi ya watoto milioni moja huko Gaza, ambao wanaendelea kuhitaji chakula na maji kwa dharura.
Tess Ingram amesema katika mahojiano siku ya Jumapili kwamba maelfu ya watoto hulala njaa kila usiku, na takriban 650,000 hawawezi kurejea shuleni licha ya makubaliano ya hivi karibuni ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa, usitishaji huo wa mapigano ni “habari njema,” kwani ulikomesha milipuko ya kila siku ambayo imekuwa ikigharimu maisha ya watoto, hata hivyo, akasisitiza kuwa usitishaji vita pekee hautoshi kuondoa njaa na kuhakikisha familia zinaweza kupata maji safi ya kunywa.
“Familia huko Gaza bado zinatatizika kila siku kuishi, na miundombinu ambayo ilitoa huduma muhimu kama vile maji na huduma ya matibabu kwa watoto imeharibiwa vibaya,” Ingram alielezea, akibainisha kuwa upatikanaji wa mahitaji haya ya kimsingi bado ni changamoto kubwa.
Ingawa amesema kwamba kiasi cha misaada inayoingia Ukanda wa Gaza kiliongezeka kidogo katika muda wa wiki mbili za kwanza baada ya kusitishwa kwa mapigano, lakini amesisitiza kuwa, misaada hiyo bado haikidhi mahitaji ya Wagaza.
Wakati huo huo, Mamlaka za Palestina katika Ukanda wa Ghaza zimetangaza kuwa utawala wa kizayuni wa Israel umeruhusu kuingizwa katika eneo hilo sehemu ndogo tu ya misaada ya kibinadamu kinyume na ilivyoafikiwa katika makubaliano ya usitishaji mapigano yanayosimamiwa na serikali ya Marekani, ambayo yalianza kutekelezwa mwezi uliopita.