Wahamiaji 45 wasio na vibali wameokolewa kwenye pwani ya mji wa Tobruk wa mashariki mwa Libya. Hayo ni kwa mujibu wa gazeti la Libya Al-Watan ambalo limesema kuwa wahamiaji hao wamekabidhiwa kwa mamlaka husika baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, wahamiaji hao waliotambuliwa kuwa ni raia 23 wa Misri na raia 22 wa Sudan wakiwa kwenye mashua ya mpira, waliokolewa na Walinzi wa Pwani ya Libya yapata kilomita 222.2 kaskazini mwa Tobruk.

Sehemu moja ya ripoti hiyo imesema kuwa, mara baada ya kuokolewa, wakimbizi hao walipewa msaada muhimu wa kimatibabu na kibinadamu na kisha wakapelekwa kwenye kituo cha kuhifadhiwa ili kukamilisha taratibu za kisheria.

Libya imekuwa kitovu cha usafiri wa wahamiaji wanaojaribu kufika Ulaya. Hali hiyo imetokea baada ya uvamizi wa NATO wa mwaka 2011 uliomng’oa madarakani Kanali Muammar Gaddafi. Mitandao ya magendo ya binadamu imeongezeka sana huku kukiwa na mgawanyiko wa kisiasa na ukosefu wa usalama nchini Libya na kuwaweka wahamiaji hao katika mazingira magumu ikiwa ni pamoja na kwenye ajali za mara kwa mara za vyombo vya baharini kwenye Bahari ya Mediterania.

Hivi sasa Libya imegawanyika vipande viwili, kati ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa na ambao makao makuu yake ni Tripoli na nyingine ni serikali ya mashariki mwa nchi hiyo unaoshirikiana na Jeshi la Taifa la Libya chini ya uongozi wa Jenerali Khalifa Haftar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *