Onyo hilo limetolewa katika ripoti mpya inayoangalia pengo la uchafuzi wa hewa au Emissions Report Gap ambayo imechapishwa hii leo na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP, ikiwa ni siku chache kabla ya kufunguliwa kwa Mkutano wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa ya Mabadiliko ya Tabianchi- (COP), COP30 utakaofanyika Belém, Brazil, wiki ijayo.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, Inger Andersen, amesema kuwa ingawa mipango ya kitaifa imeleta maendeleo fulani, kasi yake bado ni ndogo sana. “Tunahitaji kupunguza uzalishaji kwa kiwango kisichowahi kutokea ndani ya muda mfupi sana, licha ya changamoto za kisiasa duniani,” amesema, akisisitiza kuwa bado inawezekana kupunguza athari hizo kwani suluhisho zipo tayari.

Imeelezwa kuwa takribani miaka kumi imepita tangu viongozi wa dunia walipokubaliana katika Mkataba wa Paris wenye lengo la kudhibiti ongezeko la wastani wa joto duniani lisizidi nyuzi joto 2°C juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda, na ikiwezekana lisizidi nyuzi joto 1.5°C.

Hewa chafuzi kutoka kwenye uchimbaji wa mafuta ghafi inamchango mkubwa kwenye uzalishaji wa nishati ya kisukuku.

© Unsplash/Francesco Boncompagn

Kuhusu ahadi

Nchi wanachama huwasilisha mipango ya kitaifa ya kupunguza gesi chafuzi, inayojulikana kama Michango Iliyoamuliwa Kitaifa (NDCs), kila baada ya miaka mitano. Raundi ya tatu inahusu kipindi hadi mwaka 2035, lakini hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Septemba ni nchi 60 pekee (chini ya theluthi moja) ndizo zilizowasilisha mipango mipya.

Ripoti inaonesha kuwa makadirio ya ongezeko la joto duniani kufikia mwisho wa karne hii, yakizingatia utekelezaji kamili wa NDCs, ni kati ya nyuzi joto 2.3 hadi 2.5°C, ikilinganishwa na nyuzi joto 2.6 hadi 2.8°C zilizotajwa mwaka jana.

Kwa sera za sasa, makadirio ni nyuzi joto 2.8°C, chini kidogo ya makadirio ya 3.1°C mwaka uliopita.

Hata hivyo, UNEP imebainisha kuwa maboresho ya mbinu za utafiti yamechangia upungufu wa nyuzi joto 0.1°C, huku kujiondoa kwa Marekani katika Mkataba wa Paris kukitarajiwa kufuta mafanikio hayo, jambo linaloonyesha kuwa NDCs mpya hazijafanya mabadiliko makubwa.

Ili kufikia malengo ya Mkataba huo, nchi zinahitaji kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi kwa asilimia 35 kufikia mwaka 2035 ili kufikia lengo la nyuzi joto 2°C, na kwa asilimia 55 ili kufikia 1.5°C, ikilinganishwa na viwango vya mwaka 2019. Ripoti inabainisha kuwa ongezeko la wastani wa joto duniani litazidi 1.5°C kwa muda, jambo litakalokuwa gumu kulirekebisha.

Ripoti hiyo inatoa wito wa kuongeza kasi ya kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi ili kuweka uwezekano wa kurejea katika kiwango cha 1.5°C kufikia mwaka 2100.

UNEP imesisitiza kuwa kila kipimo cha nyuzi joto kinachoepukwa hupunguza madhara, hasara na athari za kiafya zinazozikumba nchi zote, hasa maskini na zilizo hatarini zaidi.

Pia imebainisha kuwa teknolojia za nishati safi kama upepo na jua tayari zinapatikana, na sasa ni wakati wa mataifa “kuekeza kwa ujasiri katika mustakabali wao kupitia hatua za haraka na shupavu za tabianchi hatua zitakazochochea ukuaji wa uchumi, afya bora, ajira zaidi, usalama wa nishati na uimara wa jamii.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *