Taarifa ya pamoja iliyotolewa leo huko Roma, Italia, Geneva Uswisi na New York, Marekani imeonya kuwa maeneo haya yamevuka viwango vya njaa kwa ulaji wa chakula, utapiamlo na vifo, huku maeneo mengine ya Sudan ambako mapigano yamepungua, hali ya upatikanajiwa chakula imeimarika kidogo.
Uchambuzi wa hivi karibuni wa Uainishaji wa Hatua za Upatikanaji wa Chakula (IPC) unaonesha kuwa watu milioni 21.2 — karibu nusu ya idadi ya watu wa Sudan — bado wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.
Hata hivyo, hali imeimarika katika baadhi ya maeneo ya Khartoum, Al Jazirah, na Sennar, ambako kupungua kwa mapigano kumeruhusu familia kurejea nyumbani, masoko kufunguliwa tena, na huduma za kibinadamu kuanza upya.
Kiwango cha utapiamlo El Fasher ni 75%
Mwanamke akiitayarishia familia yake chakula huko El Fasher, Darfur Kaskazini ambako watu wamenaswa kutokana na mapigano
Kinyume chake, El Fasher na Kadugli zimekatwa misaada ya kibinadamu na bidhaa za kibiashara kwa miezi kadhaa. Taarifa za uchunguzi zinaonesha kuwa kiwango cha Utapiamlo Mkali (GAM) kimefikia hadi asilimia 75 huko El Fasher na asilimia 29 huko Kadugli. Mlipuko wa kipindupindu, malaria na surua unaendelea kuzidisha hali ya janga, hasa kwa watoto.
Mashirika hayo yanaripoti kuwa ingawa hali katika baadhi ya maeneo ya Milima ya Nuba Magharibi imeimarika kidogo, hatari ya njaa bado ipo katika maeneo ya Darfur Kuu na Kordofan Kuu, huku maeneo 20 zaidi yako hatarini iwapo upatikanaji wa misaada hautaboreshwa.
Mapigano yasitishwe
FAO, WFP, na UNICEF wanatoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano na kuruhusu upatikanaji salama na endelevu wa misaada ya kibinadamu ili kufikisha chakula, huduma za afya na msaada wa kilimo. Wanasema kuwa bila hatua hizi — na ongezeko la ufadhili — njaa itaendelea kuenea na kusababisha vifo zaidi.
“Mapigano bado ndiyo yanayoamua nani anakula na nani hali,” amesema Ross Smith, Mkurugenzi wa Dharura wa WFP. “Tunahitaji upatikanaji usiozuiliwa na ufadhili wa haraka ili kuzuia njaa isienee.”
Mashirika haya yanasisitiza kuwa kurejesha uzalishaji wa chakula wa ndani, kufungua masoko, na kutoa huduma muhimu za afya na lishe ni muhimu kwa kuokoa maisha na kuimarisha jamii nchini Sudan.