Dar es Salaam. Mwenendo usioridhisha wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ katika mechi sita mfululizo unaweza ukawa sababu iliyochangia kwa kiasi kikubwa kusitishwa kwa mkataba wa Kocha Mkuu Hemed Suleiman ‘Morocco’.

Morocco ambaye alianza kuinoa Taifa Stars Januari 2025 akiwa Kaimu Kocha Mkuu baada ya Adel Amrouche aliyekuwa akihudumu katika nafasi hiyo kufungiwa, mkataba wake umesitishwa leo na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Kwa mujibu wa taarifa ya TFF, nafasi yake imechukuliwa na Miguel Gamondi.

“Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesitisha mkataba wa Kocha Mkuu wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Hemed Suleiman ‘Morocco.’

“Mkataba huo umesitishwa kwa makubaliano ya pande mbili, yaani TFF kwa upande mmoja na Kocha Morocco kwa upande mwingine.

“Kutokana na hatua hiyo, TFF imemteua Kocha Miguel Gamondi wa timu ya Singida Black Stars kuwa Kaimu Kocha Mkuu wa Taifa Stars.

Mazungumzo yameshafanyika kati ya TFF na Singida Black Stars kuhusu Kocha huyo kuchukua majukumu hayo mapya.

“Kocha Gamondi ndiye atakayeiongoza Taifa Stars kwenye Fainali za AFCON zitakazofanyika nchini Morocco kuanzia Desemba mwaka huu,” imefafanua taarifa ya TFF.

Kabla ya mkataba wa Morocco kusitishwa, Taifa Stars ilikuwa imecheza mechi sita mfululizo za mashindano na kirafiki bila kupata ushindi huku ikifunga bao moja tu.

Mechi hizo ni mbili za CHAN dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo ilitoka sare tasa na dhidi ya Morocco ambayo ilifungwa bao 1-0.

Baada ya hapo ikacheza mechi tatu mfululizo za kuwania kufuzu Kombe la Dunia bila kupata ushindi.

Mechi hizo ni dhidi ya Congo iliyoisha kwa sare ya bao 1-1, kisha ikafungwa bao 1-0 katika mechi dhidi ya Niger na Zambia.

Mchezo wa sita ulikuwa wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Iran ambao Taifa Stars ilifungwa mabao 2-0.

Morocco ameachana na Taifa Stars akiwa ameiongoza kufuzu AFCON 2025 na katika fainali za CHAN 2024, aliiongoza kwa mara ya kwanza kumaliza ikiwa kinara wa kundi na kufika robo Fainali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *