Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ametangaza kwenye mtandao wa kijamii wa X mnamo Novemba 4 kuachiliwa huru kwa raia wa Ufaransa Cécile Kohler na Jacques Paris. Rais ameelezea “furaha yake kubwa.”

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Cécile Kohler na Jacques Paris, raia wawili wa Ufaransa waliokuwa wanashikiliwa nchini Iran tangu mwezi Mei 2022, “wameachiliwa huru kutoka gerezani,” ametangaza Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.

“Cécile Kohler na Jacques Paris, waliokuwa wanashikiliwa kwa miaka mitatu nchini Iran, wameachiliwa huru kutoka gereza la Evin […]. Ninakaribisha hatua hii ya kwanza. Mazungumzo yanaendelea kuwezesha kurudi kwao Ufaransa haraka iwezekanavyo. Tunafanya kazi bila kuchoka katikasuala hili, na ningependa kushukuru ubalozi wetu na idara zote za serikali kwa juhudi zao,” rais ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X.

Wako “salama” katika makazi ya balozi wa Ufaransa huko Tehran, “wakisubiri kuachiliwa kwao kabisa,” amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa. “Nilizungumza na familia zao na kutuma timu kwenda nchini Iran ili kuongozana nao kibinafsi, pamoja na wafanyakazi wa ubalozi,” Jean-Noël Barrot ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X.

Paris inatoa wito kwa Tehran kupongeza “ishara ambayo imetolewa.” Cécile Kohler na Jacques Paris “wanaendelea vizuri, wanaonekana kuwa katika afya njema,” Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa amekiambia kituo cha televisheni ya France Télévisions.

“Nimempigia simu mwenzangu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, kupongeza ishara ambayo imetolewa,” ameongeza Jean-Noël Barrot.

Mnamo Septemba 24, Emmanuel Macron aliibua matumaini kwa kutaja “mtazamo thabiti” wa kuachiliwa huru kwa raia hawa wa Ufaransa, ambao Paris iliwaona kama “mateka wa serikali.” Wiki chache baadaye, Waziri wake wa Mambo ya Nje alirudia maneno haya. Lakini hatimaye Mfaransa mwingine, Lennart Monterlos, ambaye pia ni raia wa Ujerumani, aliachiliwa mapema mwezi Oktoba.

Kuachiliwa huku kunakuja baada ya Ufaransa kuachiliwa mwezi Oktoba mwanafunzi wa Iran Mahdieh Esfandiari, aliyekamatwa mapema mwaka huu huko Lyon kwa kuchapisha jumbe zinazopinga Israel kwenye mitandao ya kijamii na kushtakiwa kwa “kuunga mkono ugaidi.”

“Siku mpya,” wamewasifu mawakili

Mawakili wa raia hao wawili wa Ufaransa wamesifu “siku mpya” kwa Cécile Kohler na Jacques Paris, “wakimaliza kifungo chao kisicho halali kilichodumu kwa siku 1,277.” “Tutahakikisha kwamba siku moja haki inaweza kutolewa” kwa raia hao wawili wa Ufaransa “ambao haki zao zimekiukwa kila siku tangu Mei 7, 2022,” walisema mawakili Martin Pradel, Chirinne Ardakani, Emma Villard, na Karine Rivoallan katika taarifa iliyotumwa kwa shirika la habari la AFP.

Walihukumiwa kifungo cha miaka 20 na 17 jela mtawalia kwa kufanya ujasus kwa niaba ya Ufaransa na Israeli, Cécile Kohler na Jacques Paris wamekuwa kila mara wakisema kuwa hawa hatia. Walikuwa raia wawili wa mwisho wa Ufaransa waliokamatwa rasmi nchini Iran.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *