Kamati moja ya wabunge wa utawala wa kizayuni wa Israel imeidhinisha muswada wa kuanzisha utoaji wa adhabu ya kifo kwa Wapalestina wanaoshikiliwa kwenye magereza ya utawala huo, na kufungua njia ya kusomwa hoja hiyo kwa mara ya kwanza bungeni licha ya kuandamwa na lawama nyingi.

Hoja ya muswada huo iliyowasilishwa na chama cha Jewish Power cha waziri wa usalama wa taifa, Itamar Ben Gvir, itatoa ruhusa kwa mahakama za Israel kupitisha adhabu ya kifo kwa “mazingira ya kiutaifa” dhidi ya Wapalestina waliotiwa hatiani kwa kuwaua walowezi wa kizayuni.

Hata hivyo, sheria hiyo haiwahusu Waisraeli wanaowaua Wapalestina katika hali na mazingira sawa na hayo.

Muswada huo ulikuwa umependekezwa na vyama vya Israel vya mrengo wa kulia tangu kabla ya kuanza mauaji ya kimbari huko Ghaza mnamo Oktoba 2023, lakini wito mpya umetolewa katika miezi ya hivi karibuni wa kuuwasilisha bungeni.

Mratibu wa Wafungwa na Watu Waliopotea katika utawala wa kizayuni Gal Hirsch ambaye alihutubia kamati hiyo ya bunge kabla ya upigaji kura jana Jumatatu, alisema waziri mkuu Benjamin Netanyahu ametoa ruhusa ya kuendelezwa muswada huo. 

Muswada huo unaweza kusomwa kwa mara ya kwanza kati ya tatu katika bunge la utawala wa kizayuni wa Israel, Knesset, siku ya Jumatano.

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestna HAMAS imelaani hatua hiyo na kueleza kwamba, muswada huo “unaakisii sura chafu ya ufashisti ya utawala ghasibu wa Kizayuni”.

Hamas imetoa wito wa “kuundwa kamati za kimataifa ili kuingia katika magereza ya Israel na kuchunguza hali za wafungwa wa Kipalestina”.

Hivi sasa kuna Wapalestina wasiopungua 10,000 ambao wanashikiliwa katika magereza ya Israel, ingawa idadi halisi inaaminika kuwa kubwa zaidi, kwa sababu utawala huo ghasibu umezuia kutolewa taarifa za mahabusu wengi Wapalestina hususan wale waliotekwa nyara na vikosi vyake huko Ghaza wakati wa mauaji ya kimbari…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *