Leo ni Jumanne tarehe 13 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1447 Hijria mwafaka na 4 Novemba 2025.

Siku kama ya leo miaka 1436 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia, Bibi Fatma Zahra binti wa Mtume Muhammad SAW alikufa shahidi baada ya kuishi maisha mafupi lakini yaliyojaa baraka tele.

Baba yake ni Mtume Muhammad SAW na mama yake ni Bibi Khadija binti Khuwaylid AS. Bibi Fatma alishiriki katika medani mbalimbali za kipindi cha mwanzo mwa Uislamu akiwa bega kwa bega na Mtume wa Mwenyezi Mungu, Imam Ali bin Abi Talib AS na Waisalmu wengine waliosabilia nafsi zao kwa ajili ya dini hiyo ya Mwenyezi Mungu na alilea watoto wema, kama Imam Hassan na Hussein AS ambao Mtume (saw) amesema kuwa ni viongozi wa mabarobaro wa peponi.

Wanazuoni wamezungumzia mengi kuhusu utukufu wa Hadhrat Fatima (AS) na wamemtaja kama mfano kamili wa mwanamke Mwislamu. Kwa sababu hiyo, Mtume Muhammad (S.A.W) alimtaja Bibi Fatima (S) kinara wa wanawake wa dunia.

Bibi Fatma alisifika mno kwa tabia njema, uchamungu na elimu kubwa na alikuwa mfano na kigezo chema cha Waislamu.

Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, askari vibaraka wa utawala wa Shah uliokuwa ukitawala Iran waliivamia nyumba ya kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Ruhullah Khomeini mjini Qum na kumtia mbaroni.

Baada ya kumhamishia mjini Tehran, utawala wa Shah ulimbaidishia Imam Khomeini nchini Uturuki. Utawala wa Shah uliamua kufanya hivyo kutokana na uungaji mkono wa Imam Khomeini kwa harakati za mapambano za wananchi Waislamu wa Iran za kutaka kujitawala, uhuru na kutetea thamani za Kidini.

Lengo la kumpeleka uhamishoni Imam Khomeini lilikuwa kusimamisha mapambano yake na wananchi Waislamu wa Iran dhidi ya utawala huo kwani utawala wa Shah ulitambua kwamba kuwepo Imam nchini kunawaamsha wananchi dhidi ya utawala huo wa kidikteta.

Miaka 47 iliyopita na katika siku kama ya leo yaani tarehe 13 Aban mwaka 1357 Hijria Shamsia, kulifanyika maandamano makubwa ya wanafunzi na wanachuo mjini Tehran.

Maandamano hayo ya yalikandamizwa vibaya na askari wa utawala wa Shah na kusababisha umwagaji damu mkubwa. Katika siku kama hii ambayo ilisadifiana na kumbukumbu ya kubaidishwa Imam Khomeini huko Uturuki, kundi kubwa la wanafunzi na wanachuo, wakiwa na lengo la kulaani kitendo hicho cha mfalme Shah walikusanyika katika Chuo Kikuu cha Tehran.

Askari wa utawala wa Shah walishambulia kundi hilo la wanachuo na wanafunzi na kuwauwa shahidi wanafunzi na wanachuo wengi. Tarehe 13 Aban ina umuhimu mkubwa katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu, na ndio maana imepewa jina la “Siku ya Mwanafunzi.”

Na miaka 30 iliyopita katika siku kama hii ya leo Yitzhak Rabin, Waziri Mkuu wa zamani wa utawala wa Kizayuni wa Israel aliuawa na Mzayuni mwenye misimamo ya kufurutu ada.

Rabin alikuwa Waziri Mkuu wa Israel kuanzia mwaka 1974 hadi 1977 kwa tiketi ya Chama cha Leba. Hata hivyo aliuzuliwa wadhifa huo kwa tuhuma za ubadhirifu.

Ni muhimu kukumbusha kuwa, Yitzhak Rabin alikuwa miongoni mwa makamanda wa makundi ya kigaidi ya Kizayuni.

Yitzhak Rabin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *