Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametembelea Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) na kushuhudia kwa karibu mafanikio ya karibuni ya wanasayansi wa sekta ya nyuklia katika nyanja za afya, tiba na utengenezaji dawa za radiopharmaceutical na kisha kuzungumza na maafisa wa ngazi ya juu wa sekta hiyo.
Pezeshkian Jumapili wiki hii alikuwa na kikao na maafisa wa ngazi ya juu wa sekta ya nyuklia ya Iran na kusema: Sehemu ndogo tu ya matokeo tofauti na yasiyo ya kibinadamu ya sekta ya nyuklia ni uzalishaji wa mabomu, na kwamba sehemu iliyobaki ya tasnia hii hutumika kukidhi mahitaji ya kimsingi ya mwanadamu. Rais wa Iran ameongeza kuwa: Nia na azma ya Iran ya kupanua sekta hii si kuzalisha silaha, bali ni kudhamini mahitaji ya wananchi na kuboresha ustawi wa nchi.
Katika kikao hicho, Muhammad Eslami Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) pia ameashiria kutiwa saini makubaliano ya kujenga vinu vinane vya kuzalisha nishati ya nyuklia kwa ushirikiano na Russia na kusema: “Kwa kuzingatia mkataba mpya kati ya serikali ya Iran na Russia, Iran imeweka katika ajaenda yake ya kazi ujenzi wa vinu vinne vya kuzalisha umeme huko Bushehr na vingine vinne katika maeneo mengine ya nchi ambayo serikali itayatangaza baadaye.

Sayyid Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amesema: Haiwezekani kurutubisha urani kwa kiwango cha sifuri; urutubishaji ni mafanikio ya wanasayansi wa Iran. Vita vya siku 12 vilianzishwa dhidi yetu kutokana na urutubishaji huu,ambapo watu zaidi ya elfu moja wameuliwa shahidi; Kile ambacho hawakufanikiwa katika vita, hawawezi kukipata katika mazungumzo.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikitilia mkazo kulinda mafanikio ya sekta ya nyuklia kwa sababu inaamini kuwa sekta hii ni chombo cha kukidhi mahitaji muhimu ya wananchi, kukuza ustawi wa taifa na uhuru wa kisayansi na kiteknolojia. Sehemu kuu ya sekta ya nyuklia ya Iran Inahudumia afya na ustawi wa wananchi, ikiwa ni pamoja na katika nyanja za afya, matibabu, na uzalishaji wa dawa za radiopharmaceuticals. Teknolojia hii ina nafasi muhimu katika utambuzi na matibabu ya magonjwa, hasa saratani; na Iran imepiga hatua kubwa katika utengenezaji wa dawa za radiopharmaceuticals.
Urutubishaji wa urani ni mojawapo ya mafanikio muhimu ya wanasayansi wa Iran. Propaganda za upendeleo za vyombo vya habari vya maajinabi vyenye mfungamano na Marekani na Magharibi zimekuwa zikieneza uwongo kwamba lengo la sekta ya nyuklia ya Iran ni kutengeneza bomu la nyuklia huku Iran ikisisitiza kutumiwa teknolijia hiyo kwa malengo ya amani na ya kiraia.
Sekta ya nyuklia ya Iran ina matumizi makubwa katika nyanja za matibabu na kiuchumi, ikiwa na mchango muhimu katika kuboresha afya ya umma, kujitosheleza taifa na katika ustawi endelevu wa nchi. Iran inafanya juhudi kudhihirisha mafanikio yake ya kisayansi na kibinadamu ili kurekebisha taswira isiyo sahihi kuhusu nchi hii inayoonyeshwa katika vyombo vya habari vya Magharibi. Sekta hii si tu ni nembo ya maendeleo ya kisayansi bali ni sehemu ya utambulisho wa kitaifa wa Iran.
Matumizi muhimu zaidi ya kiuchumi ya sekta ya nyuklia ni ujenzi wa vinu vipya huko Bushehr na katika maeneo mengine hapa nchini kwa kushirikiana na Russia ili kutoa huduma ya umeme endelevu kwa wananchi na kupunguza utegemezi wa nishati ya mafuta. Iran pia imeweza kuzifanya kuwa za ndani hatua zote za mzunguko wa mafuta kuanzia uchimbaji, uboreshaji hadi uzalishaji mafuta na hivyo kupunguza gharama na kuzitegemea nchi za nje.
Hii ni katika hali ambayo kuuzwa nje tekonolojia ya Iran na bidhaa zake za nyuklia pia huchangia sehemu muhimu ya mapato ya fedha za kigeni. Dawa za radiopharmaceuticals zinazotumika katika matibabu ya nyuklia, vifaa vya mionzi, na teknolojia zinazohusiana na sekta ya nyuklia ya Iran huuzwa katika nchi za kanda hii na katika nchi mbalimbali duniani. Iran imefanikiwa kujitosheleza katika kuzalisha dawa nyingi za aina hiyo na hata kuanza kuuza nje.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaihesabu sekta ya nyuklia kama mtaji wa taifa unaohudumia maendeleo, afya na ustawi endelevu wa nchi, na pia maendeleo ya taifa, kuboresha maisha ya wananchi na kudhihirisha nafasi yake ya kisayansi duniani. Urutubishaji wa madini ya urani na kuufanya mzunguko wa mafuta ya nyuklia kuwa sekta inayotegemewa na wataalamu wa ndani ni nembo za kujitosheleza Iran na kufanikiwa katika uga wa sayansi mkabala wa mashinikizo kutoka nje.