Watu wasiopungua 20 wameuawa na wengine 34 kujeruhiwa jana Jumatatu katika mashambulizi mawili tofauti ya droni na ndege zisizo na rubani na Vikosi cha Usaidizi wa Haraka cha Kijeshi (RSF) huko katikati na magharibi mwa Sudan.

Asasi za kijamii zimetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, mashambulizi hayo yamelenga mkusanyiko wa watu katika jimbo la katikati mwa Kordofan Kaskazini na hospitali ya watoto iliyoko magharibi mwa jimbo la Darfur Kaskazini.

Kikundi cha kujitolea kinachojiita Kamati ya Muqawama ya Kordofan Kaskazini kimetangaza habari hiyo kwenye taarifa yake na kuongeza  kwa kusema: “RSF imeshambulia eneo la Al-Lulib, lililoko umbali wa takriban kilomita 15 mashariki mwa El Obeid, makao makuu ya Kordofan Kaskazini, kwa kutumia droni leo (yaani jana Jumatatu), na kuua raia 13 na kujeruhi wengine 29, baadhi yao wako katika hali mbaya.”

Katika tukio jingine, Mtandao wa Madaktari wa Sudan ambalo ni kundi jingine la kujitolea, umeripoti kwamba droni ya RSF imeshambulia hospitali ya watoto katika eneo la Kornoi huko Darfur Kaskazini na kusababisha vifo vya raia.

Kundi hilo limesema kwamba raia saba, wakiwemo wanawake na watoto wadogo wameuawa na wengine watano wamejeruhiwa vibaya. Limeongeza kuwa, watoto wawili waliokuwa wakitibiwa ndani ya hospitali hiyo ni miongoni mwa watu waliouwa kwenye shambulio hilo.

Mtandao huo umedai kuwa Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF ndivyo vilivyofanya  shambulio hilo na kuihimiza jamii ya kimataifa na mashirika ya haki za binadamu kulaani mashambulizi hayo na kuchukua hatua za haraka za kuwalinda raia. Kundi la RSF lilikuwa halijatoa tamko lolote hadi wakati tunaandaa taarifa hii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *