Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imetoa tamko juu ya wasiwasi mkubwa uliozuka kufuatia ripoti mpya kutoka El-Fasher, jimboni Darfur Kaskazini, nchini Sudan, zikielezea kufanyika mauaji ya halaiki, ubakaji, na uhalifu mwingine unaodaiwa kufanywa wakati wa mashambulizi ya Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF).

Taarifa iliyotolewa na ICC huko The Hague, Uholanzi jana Jumatatu imesema, matukio hayo ni sehemu ya mfululizo wa vitendo vya ukatili ambavyo vimeendelea kulikumba eneo la Darfur tangu Aprili 2023.

Ofisi hiyo imesema, iwapo madai hayo yatathibitishwa, yanaweza kuainishwa kama uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu chini ya Mkataba wa Roma ulioanzisha ICC.

ICC imekumbusha kuwa, kwa mujibu wa Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 1593 la mwaka 2005, mahakama hiyo ina mamlaka ya kisheria ya kuchunguza uhalifu unaoendelea kufanywa katika mgogoro wa Darfur.

Ofisi ya Mwendesha Mashtaka imesema, inaendelea na uchunguzi juu ya uhalifu unaodaiwa kufanywa tangu kuzuka kwa mapigano hayo mwaka 2023.

Katika taarifa yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ICC imesisitiza kuwa, kazi inaendelea kufanywa kwa kasi kupitia ukusanyaji wa ushahidi mashambani, mahusiano ya karibu na waathirika na asasi za kiraia, pamoja na ushirikiano ulioimarishwa na mamlaka za kitaifa na mashirika ya kimataifa.

Kuhusu matukio mapya ya El-Fasher, ofisi hiyo imesema, inachukua hatua za haraka kukusanya na kuhifadhi ushahidi muhimu utakaotumika katika mashtaka yajayo.

Aidha, ICC imeashiria hukumu iliyotolewa hivi karibuni dhidi ya kiongozi wa wanamgambo wa Janjaweed, Ali Muhammad Ali Abd-Al-Rahman al maarufu Ali Kushayb, aliyehukumiwa kwa uhalifu uliofanywa Darfur mwaka 2004, na kueleza kuwa hilo ni onyo kwa wahusika wote wa vita vya Darfur kwamba hakutakuwa na msamaha kwa uhalifu wa aina hiyo.

Ofisi ya Mwendesha Mashtaka imewataka watu binafsi na mashirika yanayohusiana na masuala ya haki na uwajibikaji kuwasilisha taarifa au ushahidi wowote unaohusiana na matukio ya hivi karibuni au ya hapo awali huko El-Fasher kupitia mfumo salama wa mtandaoni wa OTP.

Imetamatisha kwa kusema: “hakutakuwa na amani ya kweli bila haki. Wale wanaohusika na uhalifu huu watapaswa kuwajibika mbele ya sheria…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *