Madai hayo ya Rais Donald Trump yanatokana na shinikizo kutoka kwa baadhi ya wanasiasa wa Marekani kama Seneta Ted Cruz na watu mashuhuri waliodai, bila ushahidi, kuwa kuna mauaji ya Wakristo yanayoendelea nchini Nigeria. Hata hivyo, uchunguzi wa shirika la habari la Associated Press umebaini kuwa waathirika wa migogoro ya usalama nchini humo ni wa dini zote, na mara nyingi huathiriwa kutokana na maeneo wanayoishi badala ya imani zao.

Trump, kupitia ujumbe aliouweka kwenye mitandao ya kijamii Jumamosi, alidai kuwa serikali ya Nigeria inaruhusu mauaji ya Wakristo na kutishia kusitisha misaada yote kwa taifa hilo. Aliongeza kuwa Marekani inaweza kuingilia kijeshi ili kuangamiza kile alichokiita magaidi wa Kiislamu wanaotekeleza ukatili huo. Trump pia alitangaza kuiweka Nigeria kwenye orodha ya nchi zinazokiuka uhuru wa kidini, hatua ambayo imepingwa vikali na serikali ya Nigeria

Baada ya ujumbe huo Msemaji wa Rais wa Nigeria Daniel Bwala amesema madai hayo yanategemea ripoti za zamani, hasa wakati kundi la Boko Haram lilipoanzisha uasi wa kutekeleza tafsiri kali ya sheria ya Kiislamu

Nigeria yashtushwa baada ya waumini kupigwa risasi kwa wingi kanisani
Shambulio baya dhidi ya waumini wa kanisa katika mji wa Owo nchini Nigeria laiacha jamii ikiwa na hasira na maumivu.Picha: Amaka Okoye/DW

Cyril Abaku, Mtangazaji na mchambuzi wa siasa kutoka Nigeria amesema kuwa ni vyema kukawa na uwazi kwenye suala hilo. Aliongeza “Madai na tuhuma za kuingilia mambo ya ndani ya nchi yanaweza kuwepo, lakini swali la msingi ni: tunafaidika nini? Tunajua kuna vita Ukraine, na mauaji huko Gaza. Lakini kwa sisi Wanaigeria, yanayotokea hapa nchini ndiyo yanatugusa moja kwa moja. Mauaji yamefikia kiwango cha kutovumilika. Kwa hiyo, ninachoona ni kwamba tunapaswa kufikiria, ikiwa Marekani imeonyesha nia ni vipi sisi kama wananchi na serikali tunaweza kushirikiana?”

Viongozi wa dini wayapinga madai ya mateso

Viongozi wa kidini nchini Nigeria pia wamepinga madai ya mateso ya Wakristo. Joseph Hayab, aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Chama cha Wakristo Nigeria (CAN) katika jimbo la Kaduna, amesema hakuna ushahidi wa mateso hayo, ingawa amekiri kuwa serikali inapaswa kuongeza juhudi za kulinda maisha ya raia katika maeneo yenye migogoro.

Wachambuzi wa masuala ya usalama wanasema ingawa madai ya mateso ya Wakristo hayana msingi thabiti, lakini serikali ya Nigeria imeshindwa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya makundi yenye silaha.

Kwa miaka mingi, Nigeria imekumbwa na changamoto za kiusalama, hasa kaskazini mwa nchi ambapo mashambulizi hufanywa na Boko Haram na magenge yenye silaha. Mtafiti Taiwo Hassan Adebayo amesema migogoro hiyo ni tata na haiwezi kufafanuliwa kwa misingi ya kidini pekee.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *