Peru imevunja uhusiano wa kidiplomasia na Mexico siku ya Jumatatu, Novemba 3, baada ya kumpa hifadhi Waziri Mkuu wa zamani Betssy Chavez, ambaye anashtakiwa kwa jaribio la mapinduzi la Desemba 2022 lililoshindwa la rais wa zamani Pedro Castillo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Peru imetangaza.

Imechapishwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

“Tumepokea taarifa kwa mshangao na masikitiko makubwa kwamba Waziri Mkuu wa zamani Betssy Chavez, anayedaiwa kuwa mhusika mwenza wa jaribio la mapinduzi la rais wa zamani Pedro Castillo, amepewa hifadhi katika makazi ya ubalozi wa Mexico nchini Peru […] Serikali ya Peru imeamua leo kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Mexico,” Waziri wa Mambo ya Nje Hugo de Zela amesema katika mkutano na waandishi wa habari.

Uhusiano kati ya Peru na Mexico ulianza kuzorota baada ya kutimuliwa mamlakani kwa Pedro Castillo mnamo mwezi Desemba 2022, wakati Rais wa Mexico wa wakati huo Andrés Manuel López Obrador alipompa hifadhi mke na watoto wa rais wa zamani.

Tangu wakati huo, serikali ya Mexico haijatambua mamlaka yoyote ya Peru, na nchi zote mbili zimewarejesha nyumbani mabalozi wao. Licha ya mgogoro wa kisiasa, hata hivyo, nchi hizo mbili zimeendelea na biashara yao ya pande mbili.

Uhalifu unaodaiwa kuwa wa uasi

Betsy Chávez amekuwa akishtakiwa pamoja na Pedro Castillo tangu mwezi Machi 2025 kwa kosa linalodaiwa kuwa la uasi. Upande wa mashtaka unaomba kifungo cha miaka 25 jela kwa madai yake ya kushiriki, kama waziri mkuu wa zamani, katika mpango wa Pedro Castillo. Betsy Chavez aliripoti mahakamani akiwa huru, huku Pedro Castillo akiwa kizuizini tangu mwezi Desemba 2022.

Mnamo Desemba 7, 2022, Pedro Castillo alisoma ujumbe uliorushwa kwenye televisheni ukitangaza uamuzi wake wa kuvunja Bunge na kuitisha Bunge Maalum. Siku hiyo hiyo, alikabiliwa na kesi za kumwondoa madarakani kwa madai ya ufisadi. Akiwa amenyimwa usaidizi wa kijeshi, hatimaye aliondolewa mamlakani na Bunge na kisha akakamatwa alipokuwa akisafiri na familia yake kwenda ubalozi wa Mexico huko Lima. Mkewe na watoto wake wawili wamekuwa wakiishi uhamishoni nchini Mexico tangu wakati huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *